Rais wa Tanzania, Dk. John Magufuli ametoa onyo kwa viongozi wote kuanzia ngazi ya mkoa, wilaya, Halmashauri ya wilaya, mji na manispaa watakaogundulika kuhusika kuwatoza ushuru au tozo za aina yoyote wajasiriamali wadogo waliopatiwa vitambulisho rasmi kwa ajili ya kuendesha shughuli zao.
Rais Magufuli amesema hayo wakati akizungumza na wananchi jijini Dar es salaam, ikiwa ni muda mfupi tu baada ya kuongoza kikao cha viongozi wenzake wa Chama cha Mapinduzi (CCM).
Rais Magufuli ameweka wazi kuwa kiongozi yeyote atakayegundulika kuwatoza ushuru wa aina yoyote wajasiriamali wadogo wenye vitambulisho halali atachukuliwa hatua kwa mujibu wa Sheria ikiwa ni pamoja na kutolewa madarakani. Rais amesisitiza kuwa anataka wajasiliamali hao wafanye shughuli zao bila usumbufu wa aina yoyote.
Pamoja na hayo, Rais Magufuli pia amewashauri wananchi kudumisha amani, umoja na mshikamano na kujikita zaidi katika ajenda kuu, ambayo ni ujenzi wa taifa.