Home HABARI ZA AFRIKA MASHARIKI Umri usiwe kikwazo cha maendeleo

Umri usiwe kikwazo cha maendeleo

0 comment 101 views

Katika maisha kuna ambao wanabahatika kuwepo katika mazingira mazuri ambayo yanapelekea njia yao ya maendeleo kuwa rahisi na bila vikwazo vyovyote hivyo wanakuwa katika nafasi nzuri zaidi ya kujiendeleza kimasiha hasa katika masuala ya uchumi. Lakini vile vile kuwa wale ambao hawakupata bahati hiyo. Mazingira waliyoyakuta yaliwalazimu kupambana ili kutoka kimaisha. Hawa ni wale ambao hawali kama hawajahangaikia chakula chao. Kundi kubwa la watanzania wanaangukia hapa. Wengi wamelazimika kufanya kila kitu kwa bidii kubwa ili kuona matunda ya jasho lao. Lakini hadi kufikia hatua hiyo umri wa watu hawa unakuwa umeenda kwa kiasi kikubwa na wengine huona kama ni wakati wa kupumzika hivyo wanafunga milango yote ya kuwaingizia riziki.

Umri haupaswi kuwa kikwazo katika maendeleo ya mtu. Ukweli ni kwamba kuna watu wazima walio na umri wa miaka hadi thelathini wanasoma vyuoni. Hawa ni wachache walio na ujasiri wa kukubali kwamba, kutokana na sababu mbalimbali hawakupata fursa ya kujiendeleza kielimu hivyo walichukua muda zaidi kufika hapo kuliko wengine. Hili sio jambo la aibu japokuwa wengi katika jamii zetu wamekuwa na mazoea ya kutumia umri kama kikwazo katika kujiendeleza kimaisha.

Wengi wamejenga taswira ya kwamba unapaswa kuwa katika nafasi fulani kimaisha kabla hujafikia umri fulani. Taswira hii imekuwa ikiwapotosha wengi na kuwafanya waone kama hawana tena nafasi ya kujiendeleza kielimu au hata kiuchumi ili wapate kuwa katika nafasi nzuri zaidi. Jamii zetu zimekuwa hazitoi ushirikiano wa kutosha kwa makundi haya ya watu. Ni nani alisema kuwa huwezi kuendelea na elimu ukifika umri fulani? Ni kwa sababu gani watu hawa hawapewi nafasi wanayostahili katika kujenge taifa letu? Tangu lini umri umekuwa kikwazo katika masuala ya maendeleo?

Soko la ajira nalo linapaswa kutoa fursa sawa ili watu hawa wasiachwe nyuma. Kwasababu tu umri umeenda haimaanishi kuwa mtu hapaswi kunyimwa ajira. Kama vigezo vyote vinavyohitajika vipo haina maana kuweka ugumu kwa watu hawa kwani wanayo haki ya kuajiriwa kama walivyo wengine mradi tu wanakidhi matakwa yanayotakiwa. Watu hawa wanapaswa kupewa heshima wanayostahili kwa maarifa walionao na mchango wanaouleta katika jamii sio tu kwa umri walionao.

Sio jambo la aibu kujiendeleza hata kama umri wako umeenda. Kama unao uwezo wa kufanya hivyo ni vizuri kuweka bidii katika hilo na kujiendeleza. Maendeleo binafsi yanasaidia kwa kiasi kikubwa kuinua maendeleo ya nchi hivyo kundi hili la watu lisivunjike moyo na kukubali kuwa hawana nafasi katika maendeleo ya nchi.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter