Home HABARI ZA AFRIKA MASHARIKI Vikwazo 10 vya kibiashara vyaondolewa Afrika Mashariki

Vikwazo 10 vya kibiashara vyaondolewa Afrika Mashariki

0 comment 93 views

Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) zimekubaliana kuondoa vikwazo kumi vya kibiashara visivyo vya kiforodha (NTBs).

Vikwazo nane vikiendelea kushughulikiwa, na vikwazo vingine vipya vinne vimewasilishwa ili kuboresha mazingira ya uwekezaji na biashara baina ya nchi hizo.

Vilevile, nchi hizo zimekubaliana kutoza kiwango cha dola 10 za kimarekani kwa kilomita 100 kwa ajili ya matumizi ya barabara (road user charge) kwa magari ya mizigo kutoka nchi moja kwenda nyingine katika Jumuiya hiyo badala ya kila nchi kuwa na viwango vyake vya tozo.

Makubaliano hayo yamefikiwa katika Mkutano wa 42 wa Baraza la Kisekta la Mawaziri wa Biashara, Viwanda, Fedha na Uwekezaji la Jumuiya ya Afrika Mashariki (SCTIFI) uliofanyika tarehe 03 Juni, 2023 katika Makao Makuu ya Jumuiya hiyo, Jijini Arusha.

Wakizungumza baada ya Mkutano huo, Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara Dkt. Ashatu Kijaji na Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, wamesema kuwa Baraza hilo la Mawaziri wa Kisekta, limekubaliana kutoza dola 10 za kimarekani kwa kilomita 100 kwa ajili ya matumizi ya barabara kwa malori ya mizigo yanayofanya safari katika nchi wanachama badala ya kila nchi kutoza gharama zake, pamoja na kuimarisha utoaji huduma za forodha katika mpaka wa Kenya na Tanzania, kutapunguza msongamano wa malori na kuchochea ukuaji wa biashara.

Aidha, Baraza hilo limekubaliana kuondoa gharama ya viza kwa watu wanaotaka kusafiri kutoka nchi moja kwenda nyingine kwa shughuli mbalimbali zikiwemo za kibiashara, ili kukuza mahusiano miongoni mwa wakazi wa Jumuiya hiyo pamoja na kuchochea ukuaji wa biashara na uchumi wa nchi husika.

Kuhusu uondoshaji wa mizigo, Mawaziri hao walifahamishwa kuwa mizigo ya Tanzania inayosafirishwa kwenda Kenya itaendelea kuondoshwa kupitia Mfumo wa Himaya Moja ya Forodha ulioanza kutumika kuanzia mwezi Aprili 2023.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter