Naibu Waziri wa Kilimo, David Silinde amemuagiza Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Mbegu za Kilimo (ASA), Dkt. Sophia Kashenge kuharakisha mchakato wa ujenzi wa ghala la kuhifadhia mbegu zinazovunwa kwenye shamba la mbegu la Kilimi lililopo wilaya ya Nzega, mkoani Tabora.
Silinde ametoa maagizo hayo wakati wa ziara yake ya siku mbili Mei 18 na 19, 2024 Wilayani Nzega.
Katika ziara hiyo amekagua maendeleo ya uzalishaji wa mbegu kwenye shamba hilo ambalo limeshawekewa miundombinu ya umwagiliaji ili liweze kuzalisha mbegu bila kutegemea mvua.
Naibu Waziri Silinde amesema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan alikuwa na maono ya kuiwezesha nchi kuzalisha mbegu za mazao.
“Ili kuhakikisha malengo ya Rais yanatimia lazima lijengwe ghala madhubuti la kuhifadhia mbegu na kukamilika ifikapo mwezi Oktoba 2024 ambapo litahakikishia wakulima uhakika wa mbegu kama alivyokusudia na Rais,” ameeleza.
Aidha, Silinde ameagiza kuanza kwa mchakato wa upatikanaji wa kiwanda cha kusindika mbegu ndani ya shamba hilo ili kuepuka gharama za kusafirisha mbegu kwenda kiwandani mjini Morogoro na baadae kurudishwa tena kwa wakulima.
Kwa upande wake Mtendaji Mkuu ASA, Dkt. Sophia Kashenge amesema anatambua na kupongeza ushirikiano wa viongozi wa Wizara ya Kilimo kwao unaopelekea kuimarika kwa shughuli za wakala huo.
Shamba la ASA la Kilimi lina ukubwa wa hekta 11000 ambapo eneo lililotumika hadi sasa ni hekta 802.5.
Aidha, kwa sasa shamba hilo limezalisha mbegu za mahindi hekta 50, za mtama hekta 40, za alizeti hekta 10,na za choroko na hekta 250.