Home VIWANDAUZALISHAJI Makamu wa Rais atoa maelekezo kuboresha sekta ya nyuki Tanzania

Makamu wa Rais atoa maelekezo kuboresha sekta ya nyuki Tanzania

0 comment 87 views

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania, Dkt. Philip Isdor Mpango ametoa maelekezo kumi yatakayosaidia kuimarisha sekta ya nyuki ili iweze kuchangia mapato ya Serikali na kwenye uchumi wa taifa kwa ujumla.

Dkt. Mpango ametoa maelekezo haya Mei 20, 2024 kwa wadau mbalimbali wa sekta hiyo   kwenye kilele cha maadhimisho ya siku ya nyuki duniani iliyofanyika jijini Dodoma.

Katika maelekezo yake ameitaka Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kushirikiana Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) kuyatambua maeneo maalum yenye fursa za kipekee katika eneo la mkoa wa Dodoma na Singida ili kuyahifadhi kisheria na kuwaelimisha wananchi wanaoishi katika maeneo hayo ambayo yana sifa ya uoto wa vichaka vya Itigi ambavyo duniani vinapatikana Tanzania na Zambia pekee.

Dkt. Mpango ameitaka Wakala wa Misitu Tanzania (TFS) na Mfuko wa Misitu nchini(TAFF) kuwawezesha wananchi kwa kuwapatia mafunzo ya ufugaji nyuki na kuwapatia mizinga ya kisasa ili waweze kufuga kisasa.

Pia ameelekeza Taasisi ya Utafiti wa Misitu Tanzania (TAFORI) kufanya tathimini mpya ya sekta ya Misitu na Nyuki ili kuja na mipango ya kuendeleza sekta hizo.

Aidha, ameitaka Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kushirikiana na wadau wa sekta hiyo kuja na mpango maalum wa ufugaji wa nyuki, kuendeleza program ya upandaji wa miti ambapo.

Pia ameelekeza TAMISEMI kupitia Halmashauri zake zenye fursa ya ufugaji nyuki kote nchini kuajiri wataalam watakao toa huduma ya ugani kwa wananchi na Wizara inayohusika na Kilimo kuandaa mkakati wa uchavushaji katika mazao.

Kwa upande wa Wizara ya Fedha, Dkt. Mpango ameitaka kuangalia namna ya kupunguza kodi kwenye vifaa katika mnyororo wa uchakataji wa asali, huku pia akiielekeza Wizara inayohusika na Mambo ya Nje kuzielekeza Balozi za Tanzania katika nchi mbalimbali duniani kutafuta masoko ili kupata fedha za kigeni kupitia zao hili la asali.

Wakati huohuo amevitaka vyuo vya mafunzo ya nyuki nchini na Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA) kuwatumia wajasiliamali wanaofanya vizuri ili kuwafundisha wadau wengi zaidi.

Ametoa rai kwa watanzania wote   kuhamasika na kuanza kutumia mazao yatokanayo na nyuki ili kuboresha afya zao.

Awali akimkaribisha Dkt. Mpango Waziri wa Maliasili na Utalii, Angelah Kairuki amesema Sekta hiyo kupitia nyuki imekuwa na mchango mkubwa katika eneo la uzalishaji wa mazao ya chakula.

Matokeo ya tafiti mbalimbali zilizofanyika ndani ya nchi zinaonesha kuwa zaidi asilimia 80 ya mimea ya chakula inayolimwa hapa nchini huchavushwa na nyuki.

Aidha, amesema takwimu zilizopo zinaonesha kuwa sekta ya nyuki pia inachangia takribani ajira 2,000,000 hasa kwenye eneo la ufugaji nyuki, usindikaji na biashara ya mazao ya nyuki katika soko la ndani na nje ya nchi.

Amefafanua kuwa katika maadhimisho ya mwaka huu wizara yake imedhamiria kuhakikisha kuwa jamii inatambua mchango wa nyuki kwenye afya na maendeleo.

Katika maadhimisho haya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Rais Dkt. Philip Mpango pamoja na Waziri Mkuu Mstaafu, Mizengo Pinda wamepewa tuzo maalum na Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kuthamini na kutambua mchango wao kwenye sekta hiyo.

Makamu wa Rais Dkt. Philip Mpango akipokea tuzo kutoka kwa Waziri wa Maliasili na Utalii Angelah Kairuki.

Maadhimisho haya pia yamehudhuriwa na  Suleimani Jaffo Waziri wa Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Najma Giga, Makamu Mwenyekiti Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii, Dunstan Kitandula, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii.

Wengine ni wawakilishi wa Wakuu wa Mikoa wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule, Dkt. Hassan Abbasi ambae ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii na Naibu wake CP. Benedict Wakulyamba, Wakuu wa Wilaya za Dodoma, Wakuu wa Taasisi, Viongozi wa dini na Viongozi wa vyama vya siasa, huku yakitanguliwa na maonesho maalum ya wadau wa sekta ya nyuki.

Kauli mbiu ya Kitaifa ya maadhimisho haya ni “Nyuki kwa Afya na Maendeleo, Tuwatunze.” (#APIMONDIA 2027 Tanzania Ipo Tayari).”

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter