Home KILIMO Dk. Tizeba aimwagia sifa MVIWATA

Dk. Tizeba aimwagia sifa MVIWATA

0 comment 151 views

Waziri wa Kilimo, Dk. Charles Tizeba ametoa pongezi kwa Mtandao wa vikundi vya wakulima Tanzania (MVIWATA) kwa kuwa dira na muungano ulio na sauti moja yenye mshikamano, na hivyo kuwezesha mafanikio makubwa kwa wakulima nchini. Dk. Tizeba ameeleza kuwa, kwa kipindi cha miaka 25, MVIWATA imedhihirisha kuwa mtandao wenye lengo la kuwaunganisha wakulima wadogo kwa kutetea maslahi yao na kujenga mikakati ya pamoja itakayowasaidia kujikwamua kiutamaduni, kijamii na kiuchumi.

Waziri huyo ametoa pongezi hizo wakati akitoa salamu za wizara yake mbele ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ambaye alikuwa mgeni rasmi kwenye maadhimisho hayo. Mbali na hayo, Waziri Tizeba ametoa wito kwa mtandao huo kusimamia maslahi ya wakulima nchini kwa kuwa wahusika wakuu na wamiliki wa mfumo wa uzalishaji na kuwa sehemu ya mfumo wa maamuzi ya masuala yanayohusu wakulima wadogo hasa mfumo wa uzalishaji na rasilimali ardhi.

Vilevile, Dk. Tizeba amewaambia wanachama zaidi ya 2,000 walioshiriki katika kongamano hilo kuwa, wakulima wanatakiwa kueleza changamoto mbalimbali zinazowakabili ikiwa ni pamoja na kuzitafutia suluhisho la haraka.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa MVIWATA Stephen Ruvuga amepongeza serikali katika jitihada zake za kujenga uchumi wa taifa katika kuimarisha sekta ya kilimo nchini na kuongeza kuwa inapaswa kuongeza msisitizo katika kusimamia matumizi ya fedha za umma na kuongeza ukusanyaji wa mapato. Mkurugenzi huyo pia amesema japokuwa serikali imekuwa mstari wa mbele kuimarisha sekta ya kilimo, bado kuna changamoto mbalimbali zinazowakabili wakulima ikiwemo mitaji, soko la uhakika na migogoro ya ardhi.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter