Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga amekutana na kuzungumza na wadau mbalimbali kwa lengo la kuendeleza tasnia ya mbegu nchini.Kikao hicho kilichofanyika jijini Dar es salaam kimewaleta pamoja wadau kutoka Wakala wa Mbegu za Kilimo (ASA), Taasisi ya kudhibiti ubora wa mbegu (TOSCI), na Taasisi ya utafiti Tanzania (TARI) pamoja na wadau kutoka Bill & Melinda Gates kupitia kampuni ya ushauri ya mradi wa AGRI Experience.
Waziri Hasunga ameeleza kuwa serikali inalenga kuleta mapinduzi ya kilimo kwa kuongeza tija katika uzalishaji kupitia matumizi ya teknolojia ikiwemo mbegu bora. Ameongeza kuwa serikali imedhamiria kuhakikisha nchi inajitosheleza kwa mafuta ya kula na hivyo serikali inataka mradi huo kuondoa changamoto katika sekta ya mbegu kwa kuzalisha mbegu za mafuta hasa zile za alizeti na michikichi.
Aidha, Waziri huyo ametoa pongezi kwa wadau kutoka Bill & Melinda Gates kupitia kampuni ya ushauri ya mradi wa AGRI Experience kwa kushirikiana na serikali kutekeleza mradi huo.