Jumla ya vijana 268 wanatarajiwa kunufaika na programu ya Jenga Kesho iliyo Bora (Build a Better Tomorrow- BBT) baada ya kupewa vitendea kazi pamoja na barua zinazoonesha umiliki wa mashamba yenye hekari 1,340 kwa ajili ya shughuli za kilimo katika mashamba ya Chinangali, Mkoani Dodoma.
Hafla ya makabidhiano hayo imefanyika Januari 22, 2024 na kuhudhuriwa na mgeni rasmi Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu ) Prof. Joyce Ndalichako, ambapo kila mnufaika atakabidhiwa hekari tano za shamba.
Hafla hiyo pia ilihudhuriwa na Waziri wa Kilimo Hussein Bashe, David Silinde Naibu Waziri wa Kilimo, Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Gerald Mweli, Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Biashara Viwanda, Kilimo na Mifugo; na Viongozi mbalimbali wa kisekta.
Waziri Bashe amesema lengo la programu hiyo ni kupunguza umaskini, kutoa ajira kwa vijana na kutatua changamoto mbalimbali za ukosefu wa mitaji, ardhi kwa ajili ya shughuli za kilimo pamoja na teknolojia za kilimo.
Katika hatua nyingine, Serikali imewahakikishia wanufaika hao juu ya uwepo wa vitendea kazi pamoja na masoko ya uhakika ya zao la alizeti ambalo litazalishwa mara baada ya wanufaika hao kuanza shughuli za uzalishaji.
Waziri Bashe amebainisha kuwa mnunuzi wa zao la alizeti ni Bodi ya Mazao Mchanganyiko ambapo itatoa fursa ya masoko ya uhakika kwa vijana hao.
”Kati ya Dola za Marekani milioni 610 zilizotolewa na wafadhili wakati wa Mkutano wa Kimataifa wa Masuala ya Mazingira (COP28) uliofanyika Dubai mwishoni mwa mwaka 2023 zinatarajiwa kutumika katika shughuli za BBT kwa ngazi ya mashamba ya pamoja (Block farms) ikiwa ni pamoja na wakulima wadogo wanaohitaji mikopo ya riba nafuu,” amesema.
Amebainisha kuwa tayari Dola za Marekani milini 56 zimeshapokelewa kutoka katika Benki ya Dunia kwa ajili ya kutengeneza miundombinu ya umwagiliaji ya uchimbaji wa visima pamoja na vituo vya zana za kilimo.
“Serikali ina dhamira ya kuendeleza programu ya BBT ili iweze kufika katika ngazi ya Halmashauri za mikoa yote kupitia miundombinu wezeshi itakayowawezesha wakulima kuzalisha wakiwa katika mikoa yao ili kukuza Sekta ya Kilimo nchini,” amesema Waziri Bashe.
Katibu Mkuu Gerald Mweli ameeleza kuwa BBT ni programu yenye mambo matatu ndani yake ambayo ni kuwachukua vijana waliopo mtaani na kisha kuwafundisha kilimo na kuwapatia mashamba.
“Pia kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine, (SUA) kuna vijana 200 wanapewa kozi fupi ili kwenda kusimamia shughuli za kilimo. Eneo lingine ni wakulima ambapo hawa ni wakulima wanaolima kila siku lakini wanakabiliwa na changamoto za masoko, ukosefu wa vifaa na elimu ya kilimo,” amesema Mweli.
Ameeleza kuwa kabla ya kuanza kwa BBT, Wizara ilifanya tathmini na kubainisha mambo matano muhimu ya kuanza kufanyia kazi ambayo ni changamoto ya ardhi, teknolojia, elimu bora ya kilimo, mitaji na kuwa na ‘inspiration’ katika kilimo.
“Hivyo, Wizara ikaanza kufanyia kazi mambo hayo kwa kuwapa elimu ya kisasa ya kilimo ya utekelezaji wa dhana nzima ya Kilimo Biashara,” ameeleza.