Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Kahawa Tanzania (TCB) Primus Kimaryo amesema wanatarajia uzalishaji kuongezeka na kufikia tani 65,000 katika msimu mpya wa zao hilo kwa mwaka 2018/2019.
Vilevile serikali imetangaza kuzuia wanunuzi binafsi, utaratibu ambao umekuwepo kwa miaka ya nyuma na badala yake, kahawa itakusanywa na wakulima kupitia vyama vyao vya ushirika na kupelekwa mnadani. Mkurugenzi huyo akifafanua utaratibu huo mpya amesema kuwa kampuni binafsi sasa zitatakiwa kununua kahawa mnadani baada ya kukamilisha taratibu za kuomba leseni ya kununua bidhaa hiyo kwenye mnada.
Kwa upande wake, Meneja wa Chama Kikuu cha Ushirika Kilimanjaro (KNCU) Honest Temba amesema watahakikisha vyama vya msingi vinakusanya kahawa yote ya wakulima, kisha kuipeleka viwandani kwa ajili ya kukobolewa na baadae kuiwasilisha mnadani kwa ajili ya manunuzi.