Home KILIMOKILIMO BIASHARA Bashe akaribisha wawekezaji wa ndani kwenye kilimo

Bashe akaribisha wawekezaji wa ndani kwenye kilimo

0 comment 197 views

Wizara ya Kilimo imefanya Mkutano wa Wawekezaji wa Ndani uliojikita kwenye dhana ya “empowering our own’’, yaani kujijengea uwezo sisi wenyewe kama wawekezaji wa ndani.

Mkutano huo una dhamira ya kuainisha fursa zilizopo katika Sekta ya Kilimo, kupokea maoni na kukutanisha wadau na Serikali kwa ajili ya hatua zaidi za utekelezaji.

Mkutano umefanyika Desemba 18, 2023 jijini Dar es Salaam ambapo zaidi ya washiriki 200 walihudhuria Mkutano huo.

Waziri wa Kilimo Hussein Bashe ameeleza kuwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amefanya jitihada kubwa ya kuwekeza katika Sekta ya Kilimo kwa kuongeza bajeti yake ya mwaka wa Fedha 2023/24 kuwa bilioni 970 ili kuleta mapinduzi ya kilimo nchini.

“Uzalishaji endelevu unatulazimu kuzalisha chakula cha kutosha kwa matumizi ya ndani na ziada kwa ajili ya kuuza katika soko la Afrika na Dunia kwa ujumla kutokana na uhitaji mkubwa wa chakula na ongezeko kubwa la watu wanaokadiriwa kufikia bilioni mbili Duniani ifikapo mwaka 2050,” amesema Waziri Bashe.

Ameeleza kuwa kwa sasa asilimia 82 ni wakulima wadogo wenye wastani wa kulima hekari 2.5 huku asilimia 18 iliyobaki ni wakulima wanaolima mashamba makubwa yenye hekari 50-100.

“Ili kufikia hapo, lazima tufanye maamuzi kibiashara kwa kuwawezesha wakulima wadogo kwa kuweka mifumo mizuri watoke kwenye kilimo cha kujikimu na walime kibiashara,” amesema.

Amebainisha kuwa kwa kipindi cha mwaka 1970 – 2020 ukuaji wa Sekta ya Kilimo umekuwa na mabadiliko ya kisera na kiuchumi, ambapo kwa sasa tunahitaji kuwa na ukuaji endelevu.

“Mwaka 2023 tulitakiwa tukue kwa asilimia 7.1 (7.1%), kutekeleza hilo tunahitaji mitaji na uwekezaji kwa kuweka mifumo mizuri ili biashara ifanyike katika sekta, na hii litaondoa matatizo mengine ambayo yanasababishwa na hali ya maisha ya uzalishaji mdogo unaoleta umasikini,” amesema Waziri Bashe.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter