Home KILIMOKILIMO BIASHARA Vyama vya Ushirika vijijini vyatakiwa kuomba uwakala kusambaza mbolea

Vyama vya Ushirika vijijini vyatakiwa kuomba uwakala kusambaza mbolea

0 comment 110 views

Vyama vya Ushirika vijijini vimetakiwa kuendeleea kuomba uwakala wa kusambaza mbolea katika maeneo mbalimbali ili kuweza kuwafikia wakulima kwa wakati.

Naibu Waziri wa Kilimo, David Silinde amesema wakati wa ufunguzi wa Siku ya Ushirika Duniani (SUD) katika viwanja vya Nanenane vilivyopo Ipuli, Mkoani Tabora Julai 01, 2024 ambapo amemwakilisha Waziri wa Kilimo. Husein Bashe.

”Msimu wa 2021/2022 – 2023/2024 Vyama vya Ushirika vilitumika katika usambazaji wa pembejeo mbalimbali ili kuweza kuwafikia wakulima wake kwa urahisi zaidi, ambapo jumla ya shilingi 1,172,239,240,501 zilitumika kuagiza pembejeo.

Hivyo, naelekeza Vyama vya Ushirika hususan vilivyopo vijijini viendelee kuomba uwakala wa usambazaji wa pembejeo katika maeneo ya wakulima kwa wakati,” amesema Naibu Waziri Silinde.

Aidha, amezipongeza taasisi za kifedha kwa kuendelea kusaidia Sekta ya Kilimo kimtaji na kuwapatia wakulima mikopo ya jumla ya shilingi trilioni 33.159 ambapo kati ya hiyo, shilingi trilioni 3.317 ilitolewa kwenye Sekta ya Kilimo, sawa na asilimia 10 ya mikopo yote.

Ameipongeza pia Tume ya Maendeleo ya Ushirika na Wadau wake katika kuhamasisha na kuchangia mtaji katika Benki ya Taifa ya Ushirika tarajiwa kupitia uwekezaji kutoka kwa Vyama vya Ushirika na wadau, ili iweze kufikia mtaji unaotakiwa na kuwa Benki kamili ya Taifa ya Ushirika.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara Kilimo na Mifugo, Deo Mwanyika amesema kuwa Kamati hiyo inafanyia kazi suala la kuboresha sheria za ushirika na sera ili kuwezesha utekelezaji wa majukumu yake vizuri.

Viongozi mbalimbali wamehudhuria Siku ya Ushirika Duniani wakiwemo Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Tabora Deusdedith Kitwale; Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Dkt. Hussein Omar, na Mrajisi Mkuu wa Vyama vya Ushirika, Dkt. Benson Ndiege.

Kauli mbiu ya maadhimisho ni “Ushirika Hujenga Kesho iliyo Bora kwa Wote”, ambapo maadhimisho hayo yanatarajiwa kuhitimishwa Julai 06, 2024.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter