Serikali ya Tanzania imesema itaendelea kutoa kipaumbele kwa wawekezaji wenye nia ya kuwekeza kwenye viwanda vya uongezaji thamani wa mazao ya kilimo kwani ardhi ya kuzalisha malighafi za viwanda hivyo ipo.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo, Dkt. Hussein Omar amesema hayo Julai 22, 2024 alipokutana na wawekezaji na wafanyabiashara wa mazao mbalimbali ya kilimo walioletwa na Kampuni ya Yingke Law Firm ya nchini China, yenye tawi jijini Dar es Salaam.

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo, Dkt. Hussein Omar.
Dkt. Omar amewaeleza wawekezaji hao kuwa Serikali ya Tanzania chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imedhamiria kuikuza Sekta ya Kilimo ili kuleta tija zaidi kwa wakulima, huku pia vijana wakiwa sehemu ya kujishughulisha na kilimo na biashara kwa ajili ya kuwa na kipato na kutatua ukosefu wa ajira.
Aidha, Dkt. Omar amesema wawekezaji wanakaribishwa kuunga mkono Programu ya Jenga Kesho iliyo Bora (BBT) kwa kununua malighafi zitakazozalishwa na vijana wanufaika wa Programu hiyo kwa ajili ya kuzalisha bidhaa zilizoongezwa thamani.
Akizungumza kwenye kikao hicho Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Yingke Law Firm Nico Lang amesema timu hiyo ni kampuni mbalimbali za nchini China zenye wataaalamu wa udongo, mazao ya uyoga, mihogo, karanga, mahindi, ujenzi pamoja na masuala ya usafirishaji ambao wana nia ya kuwekeza kwenye Sekta ya Kilimo.
Baada ya kikao hicho wawekezaji hao walipata pia fursa ya kutembelea shamba la vijana wa BBT la Chinangali Wilayani Chamwino, mkoani Dodoma na kujionea uwekezaji unaofanywa na Wizara ya Kilimo katika kuwawezesha vijana kujikwamua kiuchumi kupitia kilimo.