Mwenyekiti wa Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF) Salum Shamte amesema kwa mujibu wa hesabu zilizofanywa na taasisi hiyo, korosho inaweza kununuliwa kwa bei iliyoelekezwa na serikali japokuwa faida wanayopata wafanyabiashara itaathirika kwa kiasi fulani. Shamte amesema hayo jijini Dar es salaam wakati akizungumza na waandishi wa habari na kueleza kuwa, ikilinganishwa na msimu wa mwaka 2017/2018, bei ya korosho katika soko la kimataifa imeshuka kwa asilimia zaidi ya 40.
“Tunampongeza Rais Magufuli kwa kusimamia kuhakikisha wakulima wanauza korosho bei inayowapa faida. Wanachama wetu wanasema inanunulika lakini faida inapungua sana kwa bei elekezi lakini sasa inapotokea jambo kama hili athari inabidi ziwe za pande mbili sio hasara kwa mkulima tu”. Amesema Mwenyekiti huyo.
Aidha, taasisi hiyo imeshauri kutumika kwa kituo cha Naliendele kufanya utafiti na kufahamu gharama halisi za uzalishaji wa zao hilo kwa msimu husika ili kurahisisha kupanga bei inayotoa faida kwa pande zote mbili. Mbali na hayo TPSF imesisitiza umuhimu wa serikali kufanya kazi kwa pamoja na sekta binafsi ili kufufua viwanda au kuzalisha vipya na vya kisasa ili kuacha kuuza ghafi kwani zao hilo linaweza kuzalisha bidhaa mbalimbali.