Waziri Mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa amemtaka Waziri wa Kilimo, Dk. Charles Tizeba kupeleka wataalamu kwenye kituo cha utafiti cha Makutupora, Dodoma ili kuchochea uzalishaji wa mbegu bora za ufuta. Majaliwa amesema hayo wakati akizungumza na wananchi wa wilayani Kondoa ambapo alikuwepo kwa ajili ya kukagua ujenzi wa kituo cha afya ikiwa ameanza ziara ya kikazi ya wiki moja mkoani humo.
“Ili mradi mikoa ya kanda ya kati inazalisha ufuta, ninamuagiza Waziri wa Kilimo ahamishe watumishi kutoka kokote ili wakae Makutupora na kuwasaidia wakulima wawe na mbegu bora zenye kutoa mafuta mengi”. Amesema Majaliwa.
Waziri Mkuu amedai kuwa kila mwaka, serikali hutumia Dola za Marekani 267 milioni kuagiza mafuta ya kula kutoa nje na kuongeza kwamba, hivi sasa wameamua kufufua mazao ya mbegu za mafuta ili mafuta ya kula yazalishwe kwa wingi hapa nyumbani.
“Sasa hivi tumeanza kufufua mazao ya mbegu za mafuta na nilianza mkoa wa Kigoma kwa kuhimiza kilimo cha michikichi. Sasa hivi niko Dodoma nahimiza ufuta na alizeti na nitaenda Singida kwa ajili ya zao hilo la alizeti”. Amesisitiza Waziri Majaliwa.
Kuhusu suala la bei, Waziri Mkuu ametoa maagizo kwa Mkuu wa mkoa huo, Dk. Binilith Mahenge kuwasiliana na wakuu wa mikoa ya Lindi na Mtwara ili kufahamu mbinu walizotumia kuhimiza zao. Pamoja na hayo, Majaliwa amemtaka asimamie na kuhakikisha kuwa katika msimu ujao, mauzo ya zao hilo yanafanyika kwa njia ya minada ili wakulima wapate bei nzuri.