Na Mwandishi wetu
Serikali imetangaza kushusha bei ya mbolea kote nchini baada ya kutoa bei elekezi ambayo ni nafuu zaidi kwa wakulima. Katika maelezo hayo bei ya juu zaidi haipaswi kuzidi Sh. 56,000 huku kwa ujumla wake viwango hivi vikitofautiana kulingana na eneo mhusika alipo.
Pia serikali imeitaka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuwachukulia hatua wafanyabiashara ambao watakiuka bei iliyoelekezwa na serikali kwa manufaa yao wenyewe. Akizungumza na wakulima wa nafaka jijini Mwanza, Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Dk. Charles Tizeba amesema hakuna mfanyabiashara atakayeruhusiwa kuuza mbolea kwa bei holela.
Waziri Tizeba ameongeza kuwa mfuko wa kilogramu 50 wa mbolea ya kupandia ni Sh. 53,000 kwa mikoa ya kanda za kati, mashariki na kaskazini, na Sh. 56,000 kwa mikoa mingine. Kwa mikoa ya kanda ya magharibi, ziwa na nyanda za juu kusini, mbolea ya kukuzia itauzwa kwa Sh. 41,000 hadi Sh. 43,000 huku kwa kanda za kaskazini mashariki na kati bei itakuwa kati ya Sh 38,000 hadi 43,000 kwa mfuko wa kilogramu 50.
Amewataka TRA, Wakuu wa Mikoa, Wilaya na Maafisa kusimamia suala hii na kuhakikisha kuwa hakuna mtu atakayeuza mbolea kwa bei ya juu kwani wakulima wamepata punguzo kubwa mwaka huu.