Vyama vya ushirika vimekuwa na mchango mkubwa sana katika kuchochea na kuleta maendeleo hususan maeneo ya vijijini. Huwezi kuitaja historia ya vyama vya ushirika nchini pasipo kukitaja chama cha kwanza cha ushirika (KNCU) kilichosajiliwa rasmi miaka ya 1930. Kutokana na mafanikio ya KNCU, viliweza kuundwa vyama vingine vya ushirika katika maeneo ya uzalishaji wa mazao ya biashara na kuungwa mkono hata wakoloni.
Kuanzia miaka ya 1970 na 1980 vyama vingi vya ushirika vilikumbwa na misukosuko mingi hali iliyopelekea baadhi ya vyama hivyo kufifia, sambamba na kupoteza mwelekeo wa kiuendeshaji.
Serikali imekuwa ikichukua hatua kadhaa kuhakikisha vyama hivi vinazidi kuwa hai ikiwa ni pamoja na kuchukua maaamuzi ya kuanzisha vyama vya ushirika wa akiba na mikopo SACCOS pamoja na ujenzi wa Chuo cha ushirika MoCUBS mwaka 1964 na baadae mwaka 2014 kukipandisha hadhi ya kuwa Chuo kikuu cha ushirika MoCu ambacho kimesaidia kuzalisha watalamu wengi kwenye taaluma ya uhasibu na ushirika.
Vyama vya ushirika vimekuwa na mchango mkubwa kwa taifa ikiwa ni pamoja na kushiriki katika harakati za kudai uhuru kwa kupigania bei nzuri ya mazao na unafuu wa pembejeo za kilimo. Baadhi ya vyama hivyo ni pamoja na Kilimanjaro Native Cooperative Union (KNCU), Victoria Federation of Cooperative Union (VFCU), Bukoba Bahaya Union (BBU) pamoja na Umoja wa Meru.
Licha ya kushiriki katika harakati za kudai uhuru bado vyama hivi vimeendelea kuwa na mchango mkubwa hata baada ya uhuru kwa kuonyesha mchango mkubwa katika kukuza uchumi na maendeleo ya jamii kwa ujumla.
Vyama vya ushirika vimekuwa na mchango mkubwa katika kuhakikisha hali za kiuchumi za wanachama na wanajamii kwa ujumla zinaimarika. Kati ya kazi muhimu zinazofanywa na vyama vya ushirika katika kupunguza umaskini na kukuza ni pamoja na huduma za masoko kwa wakulima wadogo, kuwapa sauti wanyonge, kuleta ustawi wa jamii, kutengeneza ajira, kurahisisha upatikanaji wa huduma za kifedha na uwezeshaji wa wanawake
Vyama vya ushirika vimetoa mchango mkubwa katika kuinua hali za kiuchumi za wanachama na jamii kwa ujumla. Vyama hivi vimekuwa na manufaa kwa kuwaunganisha wananchi wa hali ya chini ili waweze kujitambua, kutambua uwezo wao na kuunganisha nguvu zao katika kujiletea maendeleo.
Huduma za masoko kwa wakulima wadogo:
Asilimia 85 ya wakulima wadogo wanahitaji msaada katika uzalishaji na uuzaji wa mazao yao. Wakulima hawa tegemeo lao kubwa ni kipato kinachotokana na mauzo hivyo njia mojawapo ya kuwapunguzia umaskini ni kuwapatia masoko ya uhakika kwa mazao yao. Vyama vya ushirika wa mazao (AMCOS) vimekuwa msaada mkubwa kwa wakulima wadogo katika kutafuta masoko ya pamoja kwa kipindi cha takribani miongo sita sasa. Hivi sasa kuna vyama vya ushirika wa masoko ya mazao ya kilimo 2,769 vinavyoendeshwa na wakulima wadogo 600,000 na kuwaunganisha kwenye masoko ya bidhaa duniani.
Kuwapa nguvu wanyonge kupigania maslahi yao:
Vyama vya ushirika vinajulikana kwa uwezo wake mkubwa katika kuwaunganisha wanyonge ili waweze kusimama na kutetea haki zao na pia kuwapa uwezo wa kujadiliana na kupambana na walanguzi ili kuhakikisha kwamba wanapata bei bora ya mazao yao.
Kuleta ustawi wa jamii:
Vyama vya ushirika vimechangia sana katika kuboresha maendeleo hasa vijijini kupitia utoaji wa huduma mbalimbali. Mfano, vyama vya ushirika vimetoa mchango mkubwa katika kutoa elimu na mafunzo kwa jamii. Pia, vyama hivi vimekuwa ni jukwaa ambalo watu wanaweza kukutana na kujadiliana mambo mbalimbali kuhusu maendeleo yao. Vyama kama KNCU vimesaidia elimu ya watoto 400 wa wanachama maskini na kuwezesha huduma ya bima ya afya kwa wakulima wadogo ambao vinginevyo wangetengwa nje ya hudumu za kawaida zitokanazo na masoko.
Kuonyesha fursa mbalimbali za kutengeneza ajira:
Idadi kubwa ya vyama vya ushirika wa mazao, ushirika wa akiba na mikopo na aina nyingine za vyama vya ushirika vinatoa ajira kwa watu wengi nchi nzima. Vilevile, kuna mashirika mengi yanayovisaidia vyama vya ushirika ambayo uwepo wao unatokana na uwepo wa vyama hivi, nayo pia yanaajiri watu wengi. Pamoja na jumla ya idadi ya vyama vya ushirika 8,700 Tanzania bara, kiwango cha ajira kitokanacho na harakati za ushirika ni zaidi ya 25,000 nje ya sekta ya umma.
Kurahisisha upatikanaji huduma za kifedha:
Nchini Tanzania, kama ilivyo kwa nchi zinazoendelea, huduma za kifedha zinalenga zaidi maeneo ya mijini ambapo ndipo kwenye wateja wakubwa na biashara. Vyama vya ushirika wa akiba na mikopo vimekuwa mstari wa mbele kutoa huduma za kifedha maeneo ya vijijini na hivyo kuchochea maendeleo na kupunguza umaskini.
Kwa sasa, mfumo wa vyama vya ushirika vya akiba na mikopo unaongoza ukiwa na idadi ya vyama 5,168 vilivyosajiliwa, idadi ya wanachama ikiwa ni milioni 1.1. Kuna benki mbili za mikoa za ushirika zinazosaidia vyama vya ushirika wa akiba na mikopo (SACCOS) na vyama vya ushirika vya kilimo katika ngazi ya mkoa. Juhudi zinafanyika kuendeleza benki za ushirika za mikoa na benki ya ushirika ya Taifa – Tanzania.
Uwezeshaji wa wanawake:
Katika ulimwengu unaotawaliwa na mfumo dume, ushiriki wa wanawake katika shughuli za maendeleo bado haujafanikiwa. Katika nchi nyingi zinazoendelea ikiwemo Tanzania, vikwazo vingi vya kimila na kijadi bado vinawazuia wanawake kushiriki kikamilifu katika shughuli za kiuchumi. Uhamasishaji wa vyama vya ushirika hasa vyama vya kuweka na kukopa, umesaidia kufungua milango kwa ushiriki mkubwa zaidi wa wanawake. Vyama hivi vimewasaidia wanawake kuinua hali zao za kiuchumi na hivyo kuwaongezea nguvu na ushiriki wao katika maendeleo.
Changamoto zinazovikabili vyama vya ushirika Tanzania
Licha ya vyama hivi kuonyesha mchango mkubwa katika kuchochea maendeleo na uchumi kwa ujumla, bado vimekuwa na changamoto mbalimbali zinazopelekea uendeshaji wake kuwa duni. Baadhi ya changamoto hizo ni kama:
Kurudisha imani ya wanachama na wadau wengine:
Kama ilivyo katika historia, vyama vya ushirika Tanzania vilitawaliwa na matatizo mbalimbali ambayo yalipelekea baadhi ya wanachama kuumizwa kiuchumi. Matatizo yaliyotokana na uongozi mbovu, rushwa, ukosefu wa uwajibikaji, wizi na mengineyo yaliviacha vyama vya ushirika vikishindwa kutoa huduma bora kwa wanachama hivyo kupunguza imani ya wanachama kwenye vyama hivi. Changamoto iliyopo sasa ni kurudisha imani ya watu hawa na wadau wengine ili kuendelea kuviunga mkono vyama hivi na kushiriki katika shughuli mbalimbali za vyama vyao. Moja ya mikakati ya kurejesha kujiamini kwa wanachama, ni kuimarisha vyama vya ushirika vya msingi na kuunganisha ongezeko la thamani katika bidhaa na huduma za kifedha katika ngazi ya vijiji.
Ushiriki hafifu wa wanachama:
Vyama vya ushirika vinajulikana ulimwenguni kote kuwa ni taasisi zinazomilikiwa na kuendeshwa kidemokrasia na wanachama wake. Ili kutimiza malengo yake, vyama vya ushirika havina budi kuwa na wanachama wanaojisikia huru kushiriki kikamilifu katika shughuli zote za chama. Ni hadi hapo wanachama watakapowezeshwa kushiriki kikamilifu ndipo tutaona demokrasia ya kweli katika vyama vya ushirika.
Uwezeshaji wa wanachama hapa unachukuliwa kuwa ni kukuza uwezo wa wanachama katika kushiriki kikamilifu kwenye kufanya maamuzi katika uzalishaji na ugawanyaji wa faida zitokanazo na ushirika. Pia inamaanisha uwezo wa wanachama kutatua matatizo yao wenyewe na kuondoa vikwazo vinavyosababishwa na umaskini. Hapa nchini kumekuwepo na upungufu wa uwezo wa wanachama kusimamia mali zao jambo linalosababisha ubadhilifu kushamiri.
Ukosefu wa utawala bora na uongozi bora wa vyama vya ushirika:
Kwa kipindi kirefu, vyama vya ushirika vimekumbana na matatizo ya kiutawala yatokanayo na uongozi mbovu. Uongozi katika ushirika umehusishwa na kutokuwajibika, kukosa uaminifu na rushwa iliyokithiri. Bado kuna changamoto kubwa ya jinsi ya kuhakikisha kuwa vyama vya ushirika vinaondokana na uongozi mbovu ambao umevisababishia matatizo mengi na kuweka uongozi bora ambao utawajibika kwa wanachama. Moja ya njia bora za kukabiliana na uongozi na utawala mbovu katika vyama vya ushirika, ni mafunzo ya ujumla ya stadi za uongozi kwa wanachama. Kwa njia hii, wanachama wataweza kuweka sheria mpya za utawala katika kushughulikia matatizo kwa njia ya kidemokrasia.
Kuvifanya vyama vya ushirika kujiendesha kibiashara:
Ili kutimiza malengo yake, vyama vya ushirika havina budi kujiendesha kibiashara. Katika maeneo mengi, vyama bado vinajiendesha kimazoea na vingine bado vinamiliki vitega uchumi ambavyo haviingizi faida yoyote. Hii imepelekea vyama hivi kutokuaminika na mashirika ya kifedha hususan mabenki. Vyama vingi kwa sasa havina dhamana ya mali Bila kusisitiza vyama vijibadilishe na kujiendesha kibiashara, vyama vingi vya ushirika havitaweza kuondokana na historia na taswira mbaya iliyojengeka miongoni mwa jamii. Moja ya mikakati ya kushughulikia changamoto hii, ni mafunzo kwa wanachama katika ujuzi wa ujasiriamali ili waweze kuwa na uwezo wa kufanya tathmini ya biashara na kuwaongezea uwezo wa usimamizi. Wanachama pia wana haja ya kufanya tathmini muhimu ya miundo iliyopitwa na wakati ili waweze kuweka mifumo mipya ambayo ni ya kiushindani na gharama nafuu ili mfumo wa Ushirika uweze kukingwa dhidi ya huduma za kifedha za kinyonyaji.
Ushirika wa kibenki na bima:
Huduma za kifedha zitolewazo na vyama vya ushirika wa akiba na mikopo (SACCOS) ni mhimili muhimu sana kwa kupunguza umaskini. Lakini zaidi ya vyama vya ushirika wa akiba na mikopo (SACCOS) harakati za ushirika zina haja ya kukamilisha ajenda yake kwenye mifumo ya kifedha kwa kutengeneza mfumo kamili wa kifedha wa ushirika, wenye benki za ushirika na bima za ushirika. Aina nyingine za vyama vya ushirika zitahusishwa na ushirika wa vyama vya ushirika wa akiba na mikopo (SACCOS), benki za ushirika na bima ya ushirika ili waweze kufanya biashara inayodhibitiwa kiusawa na kidemokrasia na pia mfumo wa ushirika uweze kukingwa na huduma za kifedha za kinyonyaji.
Kutoka shirika kwenda ushirika wa kibiashara:
Wajumbe wa Mtandao wa Ushirika wa Kimataifa (International Co-operative Alliance – ICA) waliokutana mjini London mwaka 1897, walisisitiza haja ya ushirika kuwa ushirika wa kibiashara. Shirikisho la vyama vya ushirika Tanzania ni mwanachama wa ICA. Bado swala la kutoka kwenye ushirika wa kawaida kwenda ushirika wa kibiashara ni changamoto hadi sasa. Vyama vya ushirika bado havijashikamana na vyama vingine vya ushirika katika mataifa mengine. Ushirika wa kibiashara ungekuwa na faida tegemewa zaidi kwa wanachama wa kawaida kwa sababu ungekuwa na mazungumzo ya kibiashara ya kidemokrasia kama njia mbadala ya sasa ya udhibiti wa biashara ya kimataifa.
Uwezo wa kitaalamu wa kusimamia ushirika:
Chuo kikuu cha ushirika Moshi ni taasisi ya serikali inayozalisha wasimamizi wa ngazi ya juu kwa ajili ya mfumo wa ushirika nchini. Kwa sasa wataalamu wa ushirika kutoka MuCO wanakubalika na wanatoa mchango mkubwa hasa kwenye vyama vya ushirika wa akiba na mikopo (SACCOS). Kadhalika changamoto ya kuhusisha wataalamu katika usimamizi wa ushirika ichukuliwe na aina nyingine zote za vyama vya ushirika nchini na hasa katika ngazi ya vyama vya msingi vya ushirika. Vyama vya ushirika kwa sasa vinatambua kwamba ushirika wa kibiashara lazima usimamiwe kitaalamu na MuCO ipo kwa ajili hiyo.