Naibu Waziri wa Kilimo Anthony Mavunde amefanya ziara ya kikazi mkoani Tanga ambapo amezungumza Menejimenti ya Bodi ya Mkonge Tanzania baada ya kukagua ukarabati wa jengo la ofisi ya Bodi hiyo.
“Natamani kuwaona wakulima nchini wakinufaika kwa kazi wanayoifanya”, amesema Naibu Waziri.
Mavunde amesema Serikali ina malengo ya kukuza uchumi wa kaya na uchumi wa mtu mmoja mmoja kupitia zao la mkonge.
“Moja ya malengo ambayo serikali tumejiwekea ni kulipa kipaumbele zao la mkonge ambalo ni moja ya mazao ya kimkakati na tutahakikisha tunaisaidia Bodi ya Mkonge kutimiza wajibu wake ili uzalishaji uongezeke mkulima anufaike na zao hili”, amesema Mavunde.
“Nitoe rai kwa wananchi mkoa wa Tanga na maeneo yote yanayolima mkonge nchini, niwaombe muendelee kuiamini bodi yetu na kufanya nayo kazi na mjitokeze kwa wingi sana kwenye kilimo hiki, najua mlikuwa na changamoto nyingi sana ikiwemo mkonge mwingi kubaki shambani hauvunwi kwa sababu ya uwepo wa makorona mengi ya kusaidia uvunwaji”.
“Serikali tumedhamiria katika bajeti inayokuja na nimeshamuelekeza Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Mkonge kuanza mchakato mara moja wa kutangaza zabuni ya kununua makorona mengine matatu kwa ajili ya kusaidia uchakataji ili pia tuwe tumerahisisha kwa wakulima kupata sehemu ya uhakika ya uchakatwaji wa mazao yao,” amesema Mavunde.
Saddy Kambona ambae ni Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Mkonge Tanzania amesema amepokea maelekezo hayo na kusema ni hatua kubwa mbele katika kuchochea uzalishaji wa kilimo cha mkonge.
“Sisi bodi tutahakikisha mchakato huu unakwenda haraka makorona haya yaweze kununuliwa haraka zaidi. Kwa hiyo niwatie shime wananchi kuendelea kulima mkonge serikali iko pamoja nao,” amesema.
Naibu Waziri Mavunde ameitaka Menejimenti ya Bodi ya Mkonge kuleta matokeo chanya ya ukuaji wa uzalishaji wa zao la Mkonge kwa kuja na ubunifu utakaochochea kilimo hicho.
Amewasisitiza kutofanya kazi kwa mazoea na badala yake wahakikishe wanaacha alama katika kilimo cha Mkonge.
Katika ziara hiyo ya siku mbili iliyofanyika mwishoni mwa wiki Mavunde pia ametembelea Jengo la Ofisi za Bodi ya Mkonge Tanzania, kiwanda cha kutengeneza bidhaa za mkonge ambacho kinamilikiwa na Shirika la Hifadhi za Jamii (NSSF) na kusimamiwa na Kampuni Tanzu ya Sisalana, Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) na kuzungumza na wanachama wa vyama vya msingi vya ushirika (Amcos), vinavyolima mkonge mkoani Tanga.