Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amesema sekta ya kilimo inatarajiwa kukua kwa asilimia 10 ifikapo mwaka 2030 ukilinganisha na ukuaji wa sasa wa takribani 3.6%.
Rais Samia amesema Tanzania imetengeneza fursa za kitaifa kwa ajili ya mabadiliko ya mfumo wa chakula unaotarajia kuongeza uzalishaji wa chakula, kuimarisha maisha ya watu na kusaidia kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa.
Rais Samia ameeleza hayo wakati akichangia mada inayohusu masuala ya chakula katika mkutano wa Jukwaa la Uchumi Duniani (World Economic Forum) nchini Uswizi.
Rais Samia amesema katika kudhibiti mfumo endelevu wa chakula nchini, jitihada kadhaa zimefanyika ikiwemo kuanzisha mradi kwa ajili ya vijana na kuendelea kuimarisha ukuaji wa shoroba za kilimo.
Nyingine ni kuongeza bajeti ya kilimo mara nne ukilinganisha na iliyopita.
Aidha, Tanzania inatarajiwa kuwa mwenyeji wa Jukwaa la Mfumo wa Chakula Afrika mwezi Septemba kudhihirisha hayo.
Viongozi zaidi ya 50 wamehudhuria mdahalo huo kutoka Afrika, Asia, Ulaya na Marekani kwa nia ya kuongeza kasi ya ushirikiano na uwekezaji kwa maendeleo ya kila nchi.