Na Mwandishi wetu
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) Francis Assenga ameshauri wakulima wa zao la korosho kuchangamkia fursa za masoko katika nchi za Marekani, India na Vietnam. Assenga ametoa ushauri huo wakati akifungua warsha ya Siku ya Wadau wa Vyama vya Ushirika.
Mahitaji ya zao la korosho ni makubwa kwenye soko la dunia hivyo wakulima hapa nchini wanapaswa kuhakikisha kuwa wanazalisha kiasi kikubwa cha zao hilo ambalo mavuno yake kwa msimu uliopita yalikuwa tani 250,000 pekee.
Mkurugenzi huyo amesema TADB imejipanga kuratibu mfumo wa malipo ya fedha zinazotokana na mauzo ya korosho kwa njia ya Tehama, pia benki hiyo itasimamia ununuzi wa zao hilo kwa njia ya mtandao kwa kushirikiana na soko la mazao (TMX), hivyo ametaka wakulima kutumia mbinu za kisasa katika kilimo chao ili kufikia na kuvuka malengo ya mavumo yao kwa msimu unaokuja.
Naye Mkurugenzi wa Biashara wa Mikopo wa benki hiyo amesema TADB ipo tayari kutoa mikopo kwa ajili ya kunyanyua shughuli za kilimo kama ilivyolengwa na serikali.