Naibu Waziri wa Kilimo, Innocent Bashungwa amesema Tanzania na Brazil zimekubaliana kuinua kilimo cha pamba ili kuongeza tija kwa wakulima nchini. Makubaliano hayo yamekuja wakati Brazil ipo katika mageuzi makubwa ya kilimo, huku ikionyesha mafanikio makubwa katika sekta hiyo kwa nchi za Burundi, Kenya pamoja na Tanzania.
Naibu Waziri huyo amesema hayo wakati alipotembelea na kufanya ukaguzi katika mashamba ya mfano wa kilimo cha pamba katika Kituo cha Utafiti TARI-Mwanza. Bashungwa ameeleza kuwa mradi wa kuinua kilimo cha pamba unaotekelezwa na Brazil hapa nchini utajikita zaidi kuhakikisha wakulima wa pamba wanapatiwa mbegu bora na pia uzinduzi wa utafiti utamfikia ili kumsaidia kuongeza tija.
Pamoja na hayo, Naibu huyo amesema serikali imeanzisha vituo viwili vya uzalishaji pamba mbegu vipara mikoani Simiyu na Tabora huku akisisitiza kuwa serikali ya imedhamiria kuimarisha sekta ya kilimo. Vilevile, ametoa shukrani kwa Brazil kwa kutekeleza mradi huo hapa nchini, ikiwa ni ishara ya mahusiano mazuri.