Ukosefu wa maduka ya pembejeo za kilimo wilaya ya Simanjiro umewalazimu wakulima wadogo wa mazao ya chakula kutoa wito kwa serikali kuwasaidia wakidai kuwa uchache wa pembejeo unarudisha nyuma jitihada zao za kujikwamua kiuchumi kupitia shughuli za kilimo.
Wakulima hao wamesema hayo katika maadhimisho ya siku ya wakulima wilayani Simanjiro ambao wameeleza kuwa japokuwa jamii hiyo ya wafugaji haikuwa ikijikita na masuala ya kilimo hapo awali, walibadili mtazamo wao baada ya ushawishi kutoka kwa wadau wa maendeleo lakini kumekuwa na changamoto mbalimbali zinazowakatisha tama ikiwemo hiyo ya ukosefu wa pembejeo.
Akizungumzia kuhusu suala hilo, Mkuu wa wilaya ya Simanjiro Mhandisi Zephania Chaula amesema serikali imeongeza maafisa ugani na kuwaunganisha wakulima na taaasisi za fedha ili kuwawezesha kupata mikopo kwa urahisi ikiwa ni njia mojawapo ya kutatua baadhi ya changamoto zinazowakabili wakulima hao.