Home KILIMO Unakifahamu vizuri kilimo cha umwagiliaji?

Unakifahamu vizuri kilimo cha umwagiliaji?

0 comment 131 views

Imezoeleka hapa nchini kuwa wakulima hutegemea kilimo cha mvua pekee, hali ambayo inawalazimu kulima kwa misimu. Wakulima wengi hawana uelewa kuhusu kilimo cha umwagiliaji hivyo mvua inakuwa chanzo pekee cha wao kupata maji ya uhakika. Mbali na kutokuwa na elimu ya kutosha kuhusu aina hiyo ya kilimo, wakulima wengi pia huchagua kuamini kuwa kilimo hicho hufanywa na watu wenye uwezo mkubwa kifedha, jambo ambalo halina ukweli wowote.

Kabla ya yote ni vizuri kufahamu kilimo cha umwagiliaji ni nini? Hiki ni kilimo ambacho maji kutoka vyanzo vingine hupelekwa kwenye mmea, kwa maana hiyo kilimo cha umwagiliaji hakitegemei maji ya mvua pekee. Mkulima anaweza kupata maji kutoka mtoni, ziwani au kwa kufunga pampu ambayo inavuta maji kutoka kisimani au sehemu yoyote yenye maji ya uhakika. Kupitia aina hii ya kilimo, mkulima anapata uhakika wa maji katika shughuli zake hivyo hata uzalishaji nao unakuwa wa uhakika kipindi chote cha mwaka.

Kuna aina mbalimbali za kilimo cha umwagiliaji lakini kwa hapa nchini njia hizi nne ndiyo hutumika zaidi. Umwagiliaji unaweza kuwa katika njia ya mafuriko (Surface Irrigation), njia ya matone (Drip Irrigation), njia ya mtawanyo (Sprinkler Irrigation) na mwisho ni njia ya mabomba (Sub surface Irrigation). Mara nyingi njia ya mtawanyo hutumika katika mashamba makubwa wakati njia za matobe, mafuriko na mtawanyo hutumika zaidi na wakulima wadogo wadogo.

Wadau mbalimbali wa masuala ya kilimo kama vile Shirika la Maendeleo la Watu wa Japan (JICA) pamoja na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AFDB) pamoja na taasisi nyingine wamekuwa wakijitahidi kuhamasisha kilimo hiki hapa nchini. Nchi ya Japan imekuwa ikitoa misaada kwa ajili ya kuendeleza kilimo cha Umwagiliaji hapa nchini tangu mwaka 1970. Mbali na uwepo wa taasisi kama hizi ambazo zimekuwa zikijitolea kifedha, pia kuna zile ambazo zimekuwa zikitoa elimu juu ya kilimo cha umwagiliaji kupitia mikutano na program mbalimbali kwa lengo la kubadilisha mtazamo walionao wakulima wengi juu ya kilimo hicho.

Japokuwa jitihada zote hizi zimekuwa zikifanyika, aina hii ya kilimo imekuwa na changamoto mbalimbali kwa hapa nchini. Baadhi ya changamoto hizo ni pamoja na ukosefu wa mifumo bora ya kuendeleza kilimo hicho, vihifadhi bora vya maji kwa ajili ya kusaidia maendeleo ya kilimo cha umwagiliaji pia ni changamoto kubwa, upungufu wa wataalamu wa kutosha katika halmashauri na wilaya nao unarudisha nyuma kilimo hiki kwa kiasi kikubwa.

Asilimia kubwa ya watanzania wamejiajiri au wameajiriwa kupitia kilimo. Kuna kila sababu ya wadau wa kilimo kutoa elimu stahiki kuhusu kilimo cha umwagiliaji na faida zake ili watanzania wabadilike na kuanza kufanya kilimo cha kisasa zaidi.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter