Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga ameagiza wizara zote zinazohusika na vyama vya ushirika kwa akiba na mikopo (SCCULT) kuwa na Dawati la Ushirika na kuwasilisha taarifa zake kwa Mrajisi wa vyama hivyo nchini.
Waziri Hasunga ameeleza wakati wa kongamano la Vyama vya Ushirika vya Akiba na Mikopo Afrika lililofanyika jijini Mwanza alipokuwa akimuwakilisha Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa. Aidha, ameitaka Tume ya Maendeleo ya Ushirika kuwajibika na kuhakikisha vyama hivyo vinafanya kazi ipasavyo kwa kuzingatia Sheria na kanuni za ushirika (Sheria ya Ushirika namba 6 ya mwaka 2013 na kanuni zake za mwaka 2015; na kanuni za Vyama vya Ushirika Akiba na Mikopo ya mwaka 2014).
Waziri huyo amesema serikali inafanya kila jitihada kuhakikisha sekta ya ushirika inakua na kujitegemea, na hivyo haitosita kuwachukulia hatua za kisheria wale wanaokwamisha kufikia maendeleo hayo. Pia ametaja umuhimu wa ushirika wa akiba na mikopo kuwa ni jamii kuwa na mazoea ya kujiwekea akiba ya fedha mara kwa mara ili kuweza kutatua mahitaji yao mbeleni, kupitia ushirika Saccoss zimeweza kuanzishwa hadi vijijini hivyo wananchi wa kawaida kujipatia huduma. Aidha kupitia vyama hivyo, wanachama wameweza kuanzisha taasisi za fedha ambazo huwapatia mikopo kwa gharama nafuu.