Mkuu wa mkoa wa Singida Dk. Rehema Nchimbi ameagiza halmashauri za mkoa huo pamoja na maofisa ugani kuhakikisha wanatoa kalenda za msimu wa kilimo kwa wakulima na wauzaji wa pembejeo kuanzia msimu ujao.
Dk. Nchimbi ametoa agizo hilo wakati akizungumza na wakulima, maofisa ugani na wafanyabiashara wa pembejeo za kilimo kutoka Singida, Kigoma, Mtwara na Tabora ambao walikutana ili kupewa elimu sahihi ya matumizi ya viuatilifu kutoka Taasisi ya Utafiti wa Viuatilifu (TPRI) ambayo inalenga kumsaidia mkulima kufanya kilimo chenye tija.
Mbali na hayo, Dk. Nchimbi amefafanua kuwa, lengo la kufanya hivyo ni kuwadhibiti wale wenye tabia ya kuwauzia wakulima viuatilifu wakati msimu ya kunyunyizia zao husika tayari umeshapita.
Naye Kaimu Msajili wa Viuatilifu hapa nchini Habibu Mkalanga amesema wakulima wamekuwa wakipata hasara kutokana na kununua viuatilifu visivyo sahihi na kutojua wakati wa kuvitumia hali iliyopelekea ofisi yake kusitisha utoaji wa vibali wa wauzaji wasio na elimu hiyo.