Na Mwandishi wetu
Wakulima katika kata ya Ngongowele wilaya ya Liwale mkoani Lindi wametishia kususia shughuli zote za kimaendeleo mkoani hapo baada ya serikali kushindwa kukamilisha ujenzi mradi wa umwagiliaji kwa zaidi ya miaka minne.
Tangu kuzinduliwa na Waziri Mkuu Mstaafu Mizengo Pinda mwaka 2009, ujenzi huo umetumia takribani bilioni 1.03 kati ya bilioni 2.3 zilizotengwa kuukamilisha lakini mpaka hivi sasa mradi bado haujamalizika.
Mradi huo uliyokuwa umepangwa kufanyika katika awamu tatu umetumia karibu Sh.316,942,890 milioni katika hatua ya kwanza pekee ambapo serikali kupitia Mfuko wa Taifa wa Kuendeleza Umwagiliaji (NIDF) ilitoa fedha hizo. Awamu ya pili ambayo ilihusisha ujenzi wa mfereji ulifanyika mwaka 2010 uligharimu kiasi cha Sh. 346,131,268 huku awamu ya tatu ikitumia Sh.374,329,200 milioni
Utata kati ya wakulima na serikali ulianza pale ambapo fedha zilihamishwa ili kufanya mradi tofauti na ujenzi huo na kupelekea wakulima kuchukizwa na kuhoji kwanini maamuzi hayo yalifanywa bila wao kupewa taarifa.
Shirika la Maendeleo la Japan (JICA) lilitegemewa kukupesha fedha ili kuendeleza awamu ya nne ya ujenzi huu na pia kuendeleza miradi midogo midogo ya umwagiliaji. Mpaka hivi leo, mradi huu wa Liwale ambao umeunganisha vijiji vya Ngongolewe na Mikuyu unahitaji jumla ya Sh.1.2 bilioni.
Bi. Zuwena Malibishe, mkulima wilayani Liwale ambaye pia ni mnufaika wa moja kwa moja wa mradi huu ameshauri Wizara ya Kilimo na Umwagiliaji kuangalia mradi huu wa umakini zaidi ili uweze kuendelea na kukamilika ndani ya mwaka huu wa fedha.
Wakulima wengine kijijini hapo wameongeza kuwa hofu yao kubwa ni watu wachache kujinufaisha katika kipindi hiki ambapo mradi umesimama. Baadhi ya wasimamizi wasitumie nafasi hii kama mbinu ya kufuja fedha zilizotengwa kwa ajili ya mradi huu kwa matumizi yao wenyewe. Na pia wanataka waratibu wa mradi huo kutoa ufafanuzi kwanini fedha za mradi huo zimepelekwa kufanya mradi mwingine.
Mkuu wa wilaya ya Liwale Bi. Sarah Chiwamba amedhibitisha kuwepo kwa utofauti baina ya wananchi na serikali. Ameahidi kutoa ushirikiano kwa Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji wilayani hapo na punde fedha zitakapopatikana, ujenzi huu utaendelea.
Kuhusiana na miradi mingine ya umwagiliaji iliyokwama kote nchini, Waziri wa Maji na Umwagiliaji Mhandisi Gerson Lwenge amesema katika mwaka wa fedha 2017/2018 serikali haijatenga fedha za kumalizia miradi hiyo,lakini wizara yake itakuwa bega kwa bega na wadau mbalimbali wa maendeleo kuhakikisha wanatafuta fedha za kukamilisha miradi hii muhimu.