Home KILIMO Wakulima Mbeya wapewa mafunzo kilimo bora

Wakulima Mbeya wapewa mafunzo kilimo bora

0 comment 124 views

Taasisi ya Utafiti wa Kilimo (Tari) imeanza kutoa elimu kuhusu teknolojia za kisasa na mbinu bora za kilimo kwa wakulima wa Uyole mkoani Mbeya. Taasisi hiyo imelenga kutoa mafunzo hayo hasa katika uzalishaji wa mazao ya mahindi, maharage, viazi mbatata, viazi vitamu na vya lishe, ngano na maparachichi.

Mkurugenzi wa Tari-Uyole, Dk.Tulole Bucheyeki, amesema kwamba wameona kuna umuhimu wa kutoa mafunzo hayo mashambani ili kuwanufaisha zaidi wakulima tofauti na hapo awali ambapo walikuwa wakiwapa elimu na wakulima hao walikuwa hawaoni manufaa yake kwa sababu walikuwa wanapata mafunzo hayo kipindi cha mavuno.

“Sasa tumeanza na wakulima pamoja na vikundi vyao na tumeanza kuwaeleza kuwa ukilima mahindi, ngano, maharage, viazi na soya na kwa kutumia mbegu zinazozalishwa na watafiti watapata kiasi flani cha fedha kwa eneo ili wahamasike zaidi”. Amesema Mkurugenzi huyo.

Kwa upande wake Ofisa Kilimo Mtafiti wa taasisi hiyo anaehusika na Mahindi, Bonface Minja ameeleza kuwa lengo la kutoa elimu hiyo ni kuwawezesha wakulima kwenda na wakati kiteknolojia, kuongeza uzalishaji na kuunga mkono serikali na jitihada zake za kufikia uchumi wa viwanda.

“Tunawafundisha waachane na kilimo cha mazoea, matumizi sahihi ya mbolea, mbegu za kisasa, matumizi sahihi ya viuatilifu ili mazao yao yasishambuliwe na wadudu pamoja na upandaji wa kufuata vipimo sahihi”. Amesema Ofisa huyo.

Baadhi ya wakulima waliohudhuria mafunzo hayo wamesema wanatarajia kujifunza kilimo biashara ili kuongeza tija kwenye kilimo wanachofanya na vilevile kuzalisha kisasa zaidi.

 

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter