Kampuni ya Kilimo ya Organo iliyopo jijini Dar es Salaam imetoa wito kwa wakulima wadogo wa mananasi na migomba kuunda vikundi ili waweze kunufaika zaidi. Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hiyo, Ammar Mussaji, amesema lengo kubwa la kampuni hiyo ni kuwainua wakulima wadogo na wa kati na kuwawezesha kunufaika na kilimo wanachofanya.
“Tumekuwa tukifanya kazi na wakulima wakubwa ambao ni wateja wetu wengi, lakini kama kampuni ya Tanzania tumejipanga kuwainua wakulima wadogo kupitia vikundi vyao ili waweze kunufaika na huduma zetu”. Amesema Mussaji.
Pia Mkurugenzi huyo amewashauri wakulima wasio na mtaji wa kutosha na hawapo katika vikundi kujiunga katika vikundi ili iwe rahisi kwao kupata mikopo pamoja na huduma nyingine mbalimbali. Ameongezea kuwa kampuni hiyo ipo tayari kuwasaidia wakulima hao kupitia vyama kupata mikopo benki na kufanya mauzo ndani na nje ya nchi.
“Serikali ya Rais John Magufuli imeshachukua hatua mbalimbali muhimu zenye lengo la kuleta mageuzi makubwa kwenye sekta ya kilimo, hivyo ni nafasi ya wakulima wadogo hapa nchini kuanza kuchangamkia fursa hizo”. Amesema Mkurugenzi huyo.