Mkuu wa mkoa wa Tabora, Aggrey Mwanri ametoa awito kwa wakulima mkoani humo kutumia mbolea ya samadi ya ng’ombe wakati wa upandaji mazao ili kuongeza uzalishaji ikiwemo wa pamba, na hivyo kuwa na malighafi ya kutosha kwa ajili ya viwanda. Mwanri ametoa wito huo wakati akitoa elimu ya kuzingatia Sheria na Kanuni 10 za kilimo cha Pamba wilayani Nzega mkoani humo na kueleza kuwa, kilimo kinachofanyika hivi sasa pasipo kutumia samadi wala mbolea hakiwezi kuwafikisha mbali wakulima hao.
Mwanri ameeleza kuwa wawekezaji huweka mitaji yao sehemu yenye uhakika wa malighafi kwa ajili ya viwanda vyao muda wote. Aidha, amewaambia wakulima hao kuwa ofisi yake kwa kushirikiana na Chama KIkuu cha Ushirika wa Wakulima wa Pamba mkoani humo wanaendelea na taratibu za kutafuta matreka ili kucikopesha vyama vya ushirika vya msingi kwa lengo la kuviongezea ukubwa wa maeneo ya ulimaji pamba pamoja na mazao mengine.
Naye Ofisa Kilimo Mkoa wa Tabora, Modest Kaijage amewataka wakulima kuzingatia kanuni za kilimo kwani hatua hiyo itasaidia kuwa na idadi ya miche inayotakiwa kitaalamu katika shamba na hivyo kuwa na uzalishaji wenye tija.