Rais wa Tanzania, Dk. John Pombe Magufuli ametoa onyo kwa watu wanaosambaza pembejeo hewa na kuwataka kuacha tabia hiyo mara moja kwani wanakwamisha harakati za maendeleo hapa nchini. Rais Magufuli amesema hayo mkoani Njombe kabla ya uzinduzi wa barabara ya Mafinga-Nyigo-Igawa yenye urefu wa kilomita 138.7.
“Mtu anadai amesambaza magunia kadhaa ya pembejeo wakati hayapo, hatuwezi tukaendelea na nchi yenye hewa kwa sababu hatuwezi kushiba hewa. Nilipoingia madarakani niliahidi nitakuwa daktari wa kutumbua majipu zikiwemo hizi hewa ili fedha halali zitumike katika masuala mengine halali, ninajua wapo waliopata pembejeo za haki na tukishamaliza ufuatiliaji wa pembejeo watalipwa”. Amesisitiza Rais Magufuli.
Pamoja na hayo, Rais Magufuli pia ametoa pongezi kwa wananchi wa mkoa wa Njombe kwa ujenzi wa kisasa wa makazi na kutoa wito kwa mikoa mingine kuiga mfano huo.
“Tangu nimeingia Njombe nimeona nyumba zilizojengwa ni tofauti na nyumba zilizonyengwa huko kwetu kwani hakuna nyumba ya majani zote ni za bati na zimejengwa kwa matofali ya kuchoma ninafikiri mikoa mingine ambayo haijabadilika katika ujenzi wa nyumba waje wajifunze huku”. Amesema Rais Magufuli.