Waziri Mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa ametangaza ongezeko la wagonjwa 196 wa virusi vya corona nchini.
Idadi hiyo sasa ndio kubwa zaidi kushinda taifa lolote lile la Jumuiya ya Afrika mashariki.
Kati ya wagonjwa hao 174 wanatoka Tanzania Bara huku 22 wakitoka kisiwani Zanzibar (ambao tayari taarifa zao zilishatolewa na waziri wa Afya wa visiwa hivyo siku ya Jumanne).
Akizungumza na vyombo vya habari bwana Majaliwa pia ametangaza idadi ya vifo kufikia 16 ikiwa ni ongezeko la watu 6 zaidi.
Vilevile amekuwa na habari njema kwa Watanzania akisema kwamba idadi ya waliopona imeongezeka kutoka 48 hadi 167.
Tanzania kwa sasa inaongoza Afrika Mashariki kwa idadi ya wagonjwa ikifuatiwa na Kenya yenye wagonjwa 374, Rwanda 207, Uganda 79, Sudani Kusini 34 na Burundi 15.
Mji wa kibiashara wa Dar es salaam umetajwa kuongoza kwa idadi ya maambukizi nchini humo.
Licha ya mji huo kuwa kitovu cha maambukizi, Magufuli amesema jiji hilo la watu milioni sita ndio moyo wa mapato ya Tanzania.
“Wapo wengine wanatoa mawazo ya kuifunga Dar es Salaam, hili haliwezekani. Dar es salam ndio centre (sehemu) pekee ambapo collection (makusanyo) ya revenue (mapato) inapatikana kwa nchi yetu…Zaidi ya asilimia 80 ya mapato yanakusanywa Dar es Salaam,” alisema Magufuli alipokutana na viongozi wa vyombo vya ulinzi na usalama vya nchi hiyo.
Pia alisisitiza kuwa kutokana na wingi wa wakaazi wake, ilikuwa ni jambo la kutegemewa kitakwimu kwa jiji hilo kuwa na wagonjwa wengi zaidi.
Hatua hiyo inajiri baada ya shirika la Afya Duniani WHO kuikosoa Tanzania kwa kuchelewa kuchukua hatua za mapema kukabiliana na mlipuko wa ugonjwa huo.
Mkuu wa WHO wa bara la Afrika Bi Matshidiso Moeti alisema tarehe 24 Aprili kuwa kumekuwa na hofu juu ya kukua kwa kasi ya maambukizi katika taifa hilo la Afrika Mashariki.
“Kwa hakika tumeona kuwa watu kuacha kutangamana, pamoja na kupiga marufuku kwa mikusanyiko ya watu wengi kumechukua muda mrefu kufanyika na tunaamini kuwa hayo yanaweza kuwa ni moja ya mambo yaliyosababisha ongezeko la kasi la wagonjwa wa corona,” alisema Dkt Moeti katika mkutano na wanahabari.