Home LifestyleTravel Marekani, Kenya zaongoza utalii Tanzania

Marekani, Kenya zaongoza utalii Tanzania

0 comment 174 views

Marekani na Kenya zimetajwa kuwa ndio nchi zinazoongoza kwa watalii wanaotembelea Tanzania.

Utalii wa Tanzania umeanza kuongezeka ambapo takwimu zinaonyesha kuwa kuanzia Januari mpaka Julai mwaka huu Tanzania imepata watalii 742,133 sawa na ongezeko la asilimia 62.7 ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka jana ambapo kulikuwa na watalii 456,266.

Kati ya watalii 742,133 walioingia nchini, watalii 222,449 waliingia kupitia Zanzibar ambao ni sawa na asilimia 30.0 ya watalii wote.

Takwimu kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) zinaonyesha kuwa watalii walioingia nchini mwezi Julai 2022 pekee, waliongezeka hadi kufikia 166,736

ikilinganishwa na watalii 81,307 walioingia nchini mwezi Julai 2021, sawa na ongezeko la asilimia 105.1.

NBS inaonyesha kuwa idadi ya watalii walioongezeka mwezi Julai 2022 ilikuwa zaidi ya mara mbili ya watalii walioingia nchini kipindi kama hicho mwaka 2021.

“Idadi kubwa ya watalii walioingia nchini kutoka nchi zilizo nje ya Bara la Afrika kwa mchanganuo wa utaifa katika kipindi cha Januari hadi Julai 2022 walitoka Marekani ikiwa na watalii 51,301,” inasema taarifa ya NBS.

Takwimu hizo zinaonyesha nchi nyingine kuwa ni Ufaransa watalii 47,403, Ujerumani 30,817, Poland 29,004 na Uingereza 28,275.

Aidha, katika mwezi Julai 2022 pekee, idadi kubwa ya watalii walioingia nchini walitoka Marekani ambao ni 17,135, Ufaransa 12,634, Uingereza 8,586, Ujerumani 8,015 na Netherland 5,102.

Kwa upande wa watalii kutoka Barani Afrika, katika kipindi cha Januari hadi Julai idadi kubwa ya watalii walitoka Kenya ambao ni 86,22, Burundi 54,877, Malawi 27,079, Uganda 21,080 na Afrika Kusini 20,868.

Vilevile, katika kipindi cha mwezi Julai 2022 pekee idadi kubwa ya watalii walioingia nchini walitoka Kenya 16,654, Burundi 7,966, Malawi 5,113, Afrika Kusini 4,335 na Rwanda 4,035.

Aidha, kutokana na umuhimu wa Sekta ya Utalii katika kuingiza fedha za kigeni nchini, NBS imezitaka taasisi zinazotoa huduma kwa watalii kuendelea kuboresha zaidi huduma kwa lengo la kuendelea kuvutia watalii wapya na wanaokuja nchini kwa mara nyingine.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter