Home MAHOJIANO Tanzania yaishukuru Sweden

Tanzania yaishukuru Sweden

0 comment 83 views

Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Mwigulu Nchemba ameishukuru Sweden kwa misaada mbalimbali iliyoweka alama chanya katika maendeleo ya kiuchumi katika sekta ya nishati, elimu na masuala ya demokrasia.

Amesema hayo jijini Dodoma, wakati wa mkutano wake na Balozi wa Sweden nchini Tanzania, Charlotta Ozaki Macias, ulioangazia ushirikiano wa maendeleo kati ya nchi hizo mbili.

Amesema kuwa misaada inayotolewa na nchi hiyo kwa upande wa mazingira, mabadiliko ya tabia nchi, usawa wa kijinsia, elimu na nishati vinaenda sambamba na ajenda ya Taifa ya maendeleo ikiwemo Dira ya Maendeleo ya mwaka 2025.

“Utakumbuka kabla ya changamoto ya Covid 19 na Vita ya Rusia na Ukraine, uchumi wa Tanzania ulikuwa unakua kwa takribani asilimia saba, ukuaji huo ulitokana na juhudi zilizofanywa na Serikali ya Tanzania na Washirika wa Maendeleo ikiwemo Sweden, hivyo nchi yako imeweka alama katika kuinua maisha ya Watanzania”, amesema Dkt. Nchemba.

Amesema Tanzania katika kukabiliana na changamoto za kiuchumi baada ya Covid 19 na Vita ya Urusi na Ukraine, imechukua hatua kadhaa ikiwemo kutoa ruzuku kwenye mafuta na kwenye sekta ya kilimo.

Amebainisha kuwa juhudi zinazoendelea kufanywa na Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, hadi mwaka 2027 uchumi wa Tanzania unatarajia kukua kwa asilimia saba.
Kwa upande wake Balozi wa Sweden nchini Tanzania, Charlotta Ozaki Macias ameipongeza Serikali kwa kuchochea ukuaji wa uchumi, akieleza kuwa licha ya kuwepo kwa mabadiliko ya viongozi na Sera lakini bado kumekuwepo na ushirikiano ambao ni imara katika kupunguza umasikini na ujenzi wa miundombinu nchini.

Amesema nchi yake itaendeleza ushirikiano wa maendeleo hususani kwenye eneo la biashara kati ya nchi hizo mbili kwa kuwa wamefanya utafiti na kugundua kwa kiasi kikubwa mazingira ya kibiashara Tanzania ni mazuri.

Ameeleza kuwa anauzoefu mkubwa katika masuala ya kibiashara kupitia nchi nyingine kwenye kutumia usafiri wa umma katika kusaidia uchumi hususani katika miji ambayo inamsongamao wa watu na ongezeko la watu.

Leave a Comment

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter