Waziri mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa amesema kutangaza nyongeza ya mishahara ya wafanyakazi hadharani hakuna tija kwani kunaongeza gharama za maisha.
Majaliwa ametoa kauli hiyo bungeni mjini Dodoma leo Alhamisi Februari 11, 2021 katika kipindi cha maswali ya papo kwa hapo na kubainisha kuwa nia ya Serikali ni kuendelea kuboresha maslahi ya wafanyakazi nchini.
Amesema kuongeza mishahara kwa Sh20,000 halafu ikatangazwa hadharani hakuna maana yoyote kwa wafanyakazi kwani husababisha vitu vingi kupanda bila sababu.
Waziri Mkuu alikuwa akijibu swali la mbunge wa Konde (ACT-Wazalendo), Khatibu Said Haji aliyehoji ni lini Serikali itaboresha maslahi ya wafanyakazi nchini ikiwemo kupandishiwa na kuboreshewa maslahi.
Majaliwa amesema Serikali ilipoingia madarakani ilibaini kuwa kutangaza hadharani mishahara ya watumishi ni kuongeza gharama za maisha.
“Serikali inaendelea kuboresha maslahi ya watumishi katika maeneo mengine ambayo ni zaidi ya mishahara, na niwaombe wafanyakazi nchini wasikate tamaa kwa kusubiri watangaziwe hadharani,” amesema Majaliwa.