Benki ya NMB imezindua programu ya ugawaji Mizinga ya Nyuki ambapo imeanza na mizinga 500 kwa Mikoa mitatu ya Morogoro, Tabora na Njombe.
Program hiyo inalenga kusaidia jamii zilizozungukwa na rasilimali misitu na wanyamapori, kujipatia kipato mbadala ili kupunguza utegemezi wa kipato unaotokana na uvunaji ovyo wa misitu kwenye maeneo ya hifadhi.
Taarifa ya NMB inasema kuwa “kwa kutambua umuhimu wa ufugaji wa nyuki katika ekolojia ya misitu, yenye manufaa kwetu sote hasa katika juhudi za kupambana na athari za mabadiliko ya tabia nchi, tukishirikiana na Wakala wa huduma za Misitu Tanzania (TFS), chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii tumezindua program hiyo.”
Afisa Mkuu wa Wateja wakubwa na Serikali wa NMB Alfred Shao program hiyo itafikia vikundi 17 katika mikoa mitatu ambayo zaidi ya wanavikundi 300 watapata elimu ya utunzaji wa mazingira pamoja na kupata njia bora ya kisasa ya uvunaji wa asali.
NMB inaeleza kuwa program hiyo pia itaimarisha ulinzi wa makazi ya Nyuki kwani wanasaidia uwepo wa chakula kwa sababu Nyuki huchambusha mbegu ambazo baadae huzaa matunda ambayo hutumika kama chakula cha binadamu na wanyama.
Mradi huu ambao pia utatoa elimu ya Ujasiriamali na kifedha kupitia Taasisi yake ya NMB Foundation umezinduliwa mbele ya Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii Dkt. Hassan Abbas aliyeambatana na viongozi wengine wa serikali.