Na Mwandishi wetu
Naibu Waziri wa Nishati na Madini Dk. Medard Kalemani ameagiza makandarasi wanaofanya kazi ya kuunganisha umeme katika vijiji 242 mkoani Arusha kuhakikisha kuwa wanatumia wananchi waliopo katika maeneo yao ya kazi ili kuwapatia ajira pindi mradi huo ukiwa unaendelea.
Mradi huu ambao upo chini ya Mpango wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), utagharimu Sh.31 bilioni na unatekelezwa na Kampuni za Nipo Group Limited ya hapa nchini na Angelique International Limited ya India ambazo zimepewa muda wa miezi 18 ili kusambaza umeme kwa awamu tatu.
Dk. Kalemani ametaka Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kuhakikisha kuwa vijiji 33 vimeunganishwa na nishati hiyo ifikapo mwezi wa tatu mwakani na kutoa onyo kwa shirika hilo kuhusu kuzidisha gharama za kuunganisha umeme kiholela katika shule, makanisa, zahanati na misikiti.
Akieleza zaidi kuhusu taarifa ya mradi huu, Mkurugenzi wa REA, Gissima Nyamo-Hanga amesema mradi huu ukikamilika, utachochea shughuli za maendeleo na uchumi na hadi kufikia mwaka 2018 wakandarasi hao wanatakiwa kukabidhi vijiji 121 na kuwataka wananchi kutumia fursa hii kujiendeleza.