Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Selemani Jafo ameeleza kushangazwa na hali ya kusuasua kwa mradi wa ujenzi wa kituo cha mabasi cha Mbezi Luis na kutoa siku sita kupata taarifa ya kina kuhusu mradi huo. Jafo amesema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Magogoni jijini Dar es salaam na kusisitiza endapo hatopata maelezo ya kina, fedha zilizotengwa kwa ajili ya mradi huo zitapelekwa kwenye halmashauri nyingine ili zifanye shuguli za maendeleo.
“Serikali imetenga jumla ya Shilingi bilioni 105 kwa ajili ya ujenzi wa hospitali 67 za wilaya na Shilingi bilioni 50.9 za ujenzi wa kituo cha mabasi cha Mbezi Luis. Dar es salaam ni mkoa ambao umenufaika zaidi na fedha za mradi lakini mpaka sasa inasikitisha kituo cha mabasi cha Mbezi Luis kinasuasua”. Amesema Jafo.
Mradi huo ulipangwa kuanza rasmi Julai mwaka jana lakini hadi sasa bado haujaanza, kitendo ambacho kimemlazimu Waziri Jafo kutoa siku sita kwa Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda na Mkurugenzi wa jiji kumpatia maelezo ya kina kuhusu ujenzi wa kituo hicho.
“Ukiachia machinjio ya kisasa Vingunguti, ujenzi wa soko la Kisutu, soko la Mburahati, soko la Magomeni kuna mradi mkubwa wa stendi ya mabasi ya Mbezi Luis. Bahati mbaya nimetoa maelekezo katika vipindi mbali mbali miradi hii itekelezwe ndani ya muda, lakini nasikitika hatujaridhishwa na spidi ya mradi wa mabasi ya Mbezi Luis na una fedha nyingi zaidi. Natoa maelekezo mpaka Jumatano wiki ijayo tarehe 19, nipate taarifa ya mwenendo wa mradi wamefikia wapi na mkandarasi anaanza vipi kazi, na kama maelekezo haya nikiona yanasuasua, tutaziondoa fedha hizo za mradi na kupeleka kwenye halmashauri nyingine, hii naweka wazi”. Amesema Waziri huyo.