Waziri wa Maji Prof. Makame Mbarawa ametoa wito kwa watendaji wakuu wa mamlaka za maji pamoja na wahandisi wa maji kuanza kutumia mifumo ya kisasa ya TEHAMA ili kuongeza ufanisi wa mamlaka hizo katika ukusanyaji wa mapato. Waziri Mbarawa ametoa ushauri huo wakati akifungua kikao cha siku mbili cha watendaji wakuu wa mamlaka za maji na wahandisi wa mikoa kinachofanyika jijini Dodoma, lengo likiwa ni kujenga uwezo kwa watendaji hao ili waweze kutekeleza kikamilifu azma ya serikali ya awamu ya tano ya kuhakikisha kila mwananchi anafikiwa na huduma ya majisafi.
“Matumizi ya TEHAMA yatasaidia mamlaka zote kuongeza mapato yake hali itakayosaidia kuimarisha huduma zinazotolewa kwa wananchi kwa kutumia fedha zitakazokusanywa na dhamira yetu kama viongozi ni kuhakikisha kuwa wananchi wananufaika na huduma hii”. Ameeleza Prof. Mbarawa.
Mbali na hayo, Waziri Mbarawa ameweka wazi kuwa serikali imewekeza fedha nyingi kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maji ikiwemo katika jiji la Dar es Salaam ambapo Sh. 800 bilioni zimewekezwa, Arusha ikitengewa Sh. 500 bilioni huku mradi wa Shinyanga, Tabora na Nzega ukitengewa takribani Sh. 600.5. Aidha, Waziri Mbarawa amezitaka mamlaka za maji kuweka pembeni sehemu ya mapato yao kwa ajili ya kupanua huduma wanazotoa kwa wananchi.