Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Hesabu za Serikali (PAC), Naghenjwa Kaboyoka, amesema kamati yake imefurahishwa na maendeleo ya miundombinu katika jiji la Dodoma katika upande wa barabara, masoko na stendi. Mwenyekiti huyo ameongeza kuwa, Mkurugenzi wa jiji hilo Godwin Kunambi pamoja na Meya wake, Prof. Davis Mwamfupe wanastahili pongezi kwa jitihada kubwa wanazofanya kusimamia ujenzi wa miradi hiyo na kuwataka kuhakikisha inakamilika kwa wakati.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Kunambi amefafanua kuwa, miradi hiyo inategemea kukamilika hadi kufikia Septemba 30 endapo mipango yote ikienda sawa na kwamba hadi sasa miradi hiyo imekamilika kwa takribani asilimia 48.
Pia ameeleza sababu ya kuweka miradi hiyo karibu kwa mfano miradi wa soko, stendi na uwanja wa mpira kuwa ni kumrahisishia mkazi wa Dodoma kujipatia huduma mbalimbali kwa muda mchache bila ya kuzunguka bila mpangilio.
Naye Mhandisi Mkazi wa majengo ya stendi na soko, Fadhili Mosha amesema kuwa umakini wa hali ya juu unatakiwa ili kuweza kutekeleza miradi hiyo na kuepuka kurekebisha makosa kila wakati.
Aidha, baadhi ya wabunge wamepongeza hatua zilizofikiwa jijini humo upande wa serikali huku wakiitaka kuboresha miundombinu ya mikoa mingine ili kurahisisha maisha ya wananchi.