Ndege mpya tano zilizonunuliwa na serikali zinatarajiwa kuwasili nchini mwaka huu 2023, ili kuendelea kuimarisha zaidi Shirika la Ndege (ATCL).
Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa amebainisha hayo jijini Dodoma, akizungumza na waandishi wa habari.
Msigwa amesema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan, imedhamiria kuimarisha shirika hilo la ndege na kukuza utalii.
Msigwa ameeleza kuwa baadhi ya ndege hizo ambazo zitaanza kuwasili ni ndege ya mizigo aina ya Boeing 767-300, ambayo inatarajiwa kuingia nchini mwezi Machi na kufuatiwa na ndege mbili za abiria aina ya Boeing 737-9 Max, ambapo moja inatarajiwa kuingia nchini mwezi Julai na nyingine mwezi Oktoba.
Ndege nyingine ni kubwa ya abiria aina Boeing 787-8 Dreamliner, ambayo inatarajiwa kuingia nchini mwezi Novemba.
Msigwa amesema kuwa serikali inaendelea na mazungumzo na watengenezaji wa ndege ya tano aina ya Bombardier Dash 8-Q400, ambayo ni ndege ya abiria kujua itakuja lini.