Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Prof. Makame Mbarawa amesema hadi Juni 2020, miradi ya maji takribani 1,801 itakuwa imetekelezwa ambapo hadi kufikia sasa, miradi 500 ipo katika hatua mbalimbali za utekelezaji. Prof. Mbarawa amesema hayo wakati wa kuweka jiwe la msingi katika mradi wa majisafi na majitaka jijini Arusha ambapo ameeleza kuwa miradi hiyo imeelekezwa katika maeneo mbalimbali yanayokumbwa na tatizo la maji ili kuhakikisha kuwa lengo la serikali la kuwapatia wananchi majisafi linatimia.
“Miradi hii inatuhakikishia kuwa ifikapo 2020 kupitia ilani ya CCM ambayo inasema watu wote wanaoishi katika mikoa wapate maji kwa asilimia 95, wilaya asilimia 90 na vijiji asilimia 85”. Amesema Waziri Mbarawa.
Mradi huo uliozinduliwa jijini Arusha wenye thamani ya Sh. 520 bilioni ni moja kati ya miradi inayotekelezwa hivi sasa ambapo Waziri huyo amewahakikishia wananchi kuwa, maji yatapatikana muda wote.