Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Atashasta Nditiye ameeleza Bunge kuwa reli mpya ya kisasa maarufu kama Standard Gauge itajengwa kwenye mahandaki na kutakuwa na madaraja yenye mihimili iliyoinuliwa juu zaidi ili kuepuka changamoto ya mafuriko ya mara kwa mara katika eneo la Kidete-Godegode, Gulwe na Msagali. Mahandaki hayo manne yatakuwa na umbali wa kilomita 2.75 na madaraja yenye uwazi wa mita 400.
Nditiye ametoa ufafanuzi huo wakati akijibu swali la Mbunge wa Mpwapwa, George Lubuleje aliyehoji serikali ina mpango gani kujenga SGR kutoka Dar es Salaam hadi Kigoma. Naibu Waziri huyo ameeleza Bunge kuwa, ili kuepuka uharibifu, reli ya kisasa haitokuwa jirani na mito bali itapitia vilimani mbali na kingo za mito ya Mkondoa na Chinyasungwi.
Vilevile, Nditiye amesema kwa kushirikiana na serikali ya Japan kupitia shirika la JICA, wamekamilisha upembuzi yakinifu kuhusu upatikanaji wa suluhisho la kudumu katika eneo la Kidete-Godegode, Gulwe na Msagali ambalo hupatwa na mafuriko mara kwa mara. Kiongozi huyo pia amelifahamisha Bunge kuwa, mazungumzo yanaendelea kati ya Tanzania na Japan ili kupata fedha zitakazotumika kutatua tatizo hilo.