Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Ashatu Kijaji pamoja na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk. Damas Ndumbaro wameagiza watendaji wa kituo cha pamoja cha forodha Mpakani-Horohoro kuwasilisha nyaraka (ikiwemo mkataba) za ujenzi wa kituo hicho kufuatia kutoridhishwa na miundombinu ambayo wamedai haijakidhi viwango.
Manaibu hao wamesema hayo walipofanya ziara ya kukagua kituo hicho ambacho kimeshindwa kufunguliwa rasmi kwa tangu mwaka 2015. Dk. Kijaji amesema kuwa, kituo hicho hakina mawasiliano upande wa Tanzania na Kenya hivyo kutokidhi vigezo vya kuwa kituo cha pamoja cha forodha kati ya nchi hizo mbili.
Baadhi ya kasoro zilizobainika katika ziara hiyo ni pamoja na kamera maalum kwa ajili ya usalama zinazotakiwa kufanya kazi ni zaidi ya 14 lakini zinazofanya kazi mpaka sasa ni 4 pekee, hivyo inapelekea usalama wa kituo hicho kutokuwa wa uhakika.
Naibu Waziri huyo wa Fedha na Mipango pia ameagiza utaratibu wa wakazi wa Horohoro kufuata huduma za TRA katika wilayani Muheza kusitishwa mara moja na badala yake, watumishi kutoka mamlaka hiyo waende kuwahudumia wananchi katika Wilaya ya Mkinga ili kuondoa usumbufu kwa wafanyabiashara pindi wanapotaka kulipa kodi au kutafuta huduma za masuala ya forodha.
Naye Dk. Ndumbaro ametaka fedha zitazotumika kwa ajili ya kuagiza maji kila mwezi kutumika kuchimba kisima cha kudumu katika eneo hilo ili kuokoa fedha.