Ili kushinikiza Mamlaka ya Udhibiti wa Usafirishaji wa Nchi Kavu na Majini (SUMATRA) kutekeleza agizo liliotolewa na Waziri Mkuu, wadau wa sekta ya usafirishaji abiria pamoja na chama cha madereva wa mabasi nchini wametishia kusitisha huduma za usafiri nchi nzima endapo SUMATRA isipokaa pamoja nao na kupitia sheria na kanuni mpya ili kutafuta suluhu katika vipengele ambavyo pande hizo mbili zinatofautiana.
Akizungumza kwa niaba ya madereva, Mwenyekiti wa Chama cha madereva wa mabasi Shabani Mdemu amesema SUMATRA haikupaswa kutoza faini kubwa zilizopo katika sheria na kanuni mpya bila ya pande hizo mbili kujadiliana kama alivyoagiza Waziri Mkuu Kassim Majaliwa.
Akizungumzia suala hilo, Katibu Mkuu wa Chama cha Wamiliki wa Mabasi Tanzania(TABOA) Enea Mrutu ametoa wito kwa madereva hao kusitisha mpango huo na kudai kuwa tayari TABOA ipo katika mchakato wa kuonana na viongozi ili kujadili changamoto mbalimbali zilizopo katika sekta ya usafirishaji.