Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bandari ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) Mhandisi Deusdedit Kakoko ametoa wito kwa wahandisi wazalendo kuchangamkia fursa za uwekezaji katika miradi mbalimbali iliyopo chini ya mamlaka hiyo hapa nchini. Mhandisi Kakoko ametoa ushauri huo wakati wa warsha iliyoandaliwa na Chama cha Wataalamu Washauri wa Wahandisi na kuongeza kuwa hivi sasa ni wakati muafaka kuchangamkia fursa zinazopatikana bandarini. Kakoko amesema japokuwa malengo ya TPA kwenye warsha hiyo ni kuzungumzia uwepo wa miradi mikubwa ya maendeleo, wamechukua nafasi hiyo ili kuendeleza bandari kwa huduma zao kupitia miradi iliyopo na kuwashawishi wachangamkie fursa zilizopo.
“Bandarini kuna fursa ya kazi za ujenzi wa miundombinu katika nyanja zote kama ujenzi wa mitambo, umeme, mafuta, gesi na TEHAMA”. Amedai Mhandisi Kakoko.
Mbali na hayo, Mkurugenzi huyo ameeleza kuwa, changamoto kubwa kwa sasa ni kushindwa kuchukua hatua za makusudi za kuchangamkia fursa kwa makampuni ya ujenzi ya ndani, uwezo mdogo wa wahandisi, idadi ndogo ya wataalamu wenye weledi pamoja na vikundi vya taaluma kutofanya kazi kwa pamoja. Akiwasilisha mkakati mpya wa kuboresha miradi ya miundombinu ya TPA, Mhandisi Kakoko amewashauri wahandisi wazawa kuendeleza mafunzo ya pamoja mara kwa mara.
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Mipango ya Miundombinu na Uwekezaji TPA, Mhandisi Allen Banda amedai kuwa miradi mingi imefanikiwa kwa sababu ya uwepo wa wahandisi washauri.
“Nachukua fursa hii kushauri wahandisi washauri wazalendo wale wenye uzoefu kushirikiana na wengine ili kubadilishana uzoefu huo”. Amesema Mhandisi Banda.