Inategemewa kuwa baada ya miaka tisa kutoka sasa (2025), asilimia 80 ya Watanzania watakuwa wanatumia nishati safi ya kupikia.
Hiyo, itakuwa ni matokeo ya utekelezaji wa Mkakati wa Nishati safi ya Kupikia kitaifa unaosimamiwa na Kamati ya wataalam iliyoundwa na Maafisa Waandamizi kutoka katika Wizara na Taasisi mbalimbali.
Kamati hiyo imefanya kikao kazi katika Ofisi za Wakala wa Nishati Vijijini ( REA )jijini Dodoma Februari 5,2025 kujadili mkakati huo.
Kamati imejadili utekelezaji wa mkakati huo wenye lengo la kuhakikisha asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati safi ya kupikia ifikapo 2034.
Katika kikao hicho, Maafisa Waandamizi wamepitia taarifa mbalimbali za utekelezaji na kutoa mapendekezo yaliyolenga kuboresha nyaraka hizo kabla ya kuziwasilisha katika Kamati ya Makatibu Wakuu.
Matumizi ya Nishati safi ya Kupikia ni Ajenda ya Kitaifa inayohakikisha wananchi wanaondokana na matumizi ya nishati isiyo safi ikiwemo kuni na mkaa.
Mwenyekiti wa kikao kazi hicho, Omari Ilyas ambaye ni Mkurugenzi Msaidizi Uratibu wa Shughuli za Serikali kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu amesisitiza utekelezaji wa mkakati huo usiwe na kikwazo hivyo bajeti za utekelezaji wa mkakati wa nishati safi ya kupikia zinapaswa kutengwa.
“Wizara na taasisi zote kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wanatakiwa kutekeleza mkakati huu kwa kiwango kikubwa na bajeti zitengwe ili utekelezaji wa mkakati uwe na tija,” amesema Ilyas.
Kamati hiyo pia ilipokea wasilisho na kufanya maboresho ya rasimu ya mwongozo wa uratibu wa utekelezaji wa Mkakati wa Nishati Safi ya Kupikia iliyoainisha majukumu ya wadau wote ili kufanikisha uratibu husika kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kushirikiana na Wizara ya Nishati.
Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan ndie kinara wa ajenda ya nishati safi ya kupikia nchini na Afrika nab ado anaendelea kuipeleka ajenda hiyo Kimataifa ili kuhakikisha watu wanapika katika mazingira salama kiafya na kimazingira.
Agosti 2024, Naibu Waziri na Waziri wa nishati Dkt. Dotto Biteko alisema suala la nishati safi ya kupikia imekuwa ajenda muhimu nchini na duniani kote na Rais Samia amekuwa ni kinara wa ajenda hiyo Afrika kwa kuibeba kuanzia mwezi Novemba 2022.
Alisema lengo la Serikali ni kuhakikisha kuwa kila Mtanzania anapika katika mazingira salama na kwamba hatua hii itawezekana kwa kupatikana kwa nishati safi ya kupikia iliyo nafuu, inayopatikana na kutumika kwa urahisi.
Alisema Wizara ya Nishati itaendelea kutoa kipaumbele ajenda hiyo kwa namna mbalimbali ikiwemo kuanzisha Kitengo maalum cha usimamizi wa nishati hiyo.
Alitoa wito kwa vongozi wa Serikali, siasa, dini na jadi waliopo katika maeneo mbalimbali kuunga mkono ajenda hiyo yenye nia njema ya kumkomboa kila Mtanzania na kwamba kwenye majukwaa yao wasiliache nyuma suala hilo.
“Tuhakikishe watu tunaowaongoza wanaelewa vyema umuhimu wa matumizi ya nishati safi ya kupikia. Kwa kampuni zinazowajibika katika jamii zao kupitia Corporate Social Responsibilities (CSR) niwahimize kushirikiana na Serikali katika kutekeleza mkakati kwa vitendo ka kugawa vifaa vya nishati safi ya kupikia kwa wenye uhitaji. Naamini tukishirikiana wote kwa pamoja tunaweza,” alisema Dkt. Biteko.
Alieleza kuwa, takribani watu bilioni 2.4 hawatumii nishati safi duniani, kati ya hao milioni 933 wanatoka Afrika na kwa mwaka duniani watu milioni 3.7 wanakufa na vifo ni asilimia 60 wakiwemo wanawake na Watoto.