Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Mhandisi Kapuulya Musomba amesema kutumia gesi asilia katika uzalishaji wa umeme kumeokoa Sh. 23.56 trilioni (Takribani Dola za Marekani 10.29 bilioni) ambazo zingetumika kununua mafuta nje ya nchi ili kuzalisha umeme kuanzia 2004 hadi Septemba mwaka huu. Musomba amesema hayo wakati akiwasilisha taarifa kuhusu mchango wa gesi katika kuzalisha umeme kwa wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini.
“Kwa kipindi cha kuanzia mwaka 2004 hadi Septemba 2018, gesi asilia kiasi cha futi za ujazo bilioni 381 kilitumika kuzalisha umeme pekee ambapo hadi kufikia Septemba 2018, mitambo yenye uwezo wa kuzalisha umeme wa jumla ya megawati 831 kwa siku kutokana na gesi asilia imewekezwa nchini”. Ameeleza Kaimu Mkurugenzi huyo.
Naye Waziri wa Nishati Dk. Medard Kalemani amesema hadi kufikia sasa kiasi cha gesi kilichopatikana nchini ni futi za ujazo trilioni 57.54 trilioni ambapo kati ya hizo, futi za ujazo 8.96 trilioni zimepangwa kutumika katika uzalishaji umeme hadi kufikia mwaka 2046. Dk. Kalemani ameongeza kuwa serikali inaendelea na utekelezaji wa miradi mbalimbai ya uzalishaji umeme kwa kutumia gesi asilia ikiwemo mradi wa kupanua kituo cha kuzalisha umeme cha Kinyerezi I.
“Tunatarajia pia kutekeleza mradi wa Somanga Fungu utakaozalisha umeme wa kiasi cha megawati 330 kwa kutumia gesi asilia unaotarajiwa kukamilika mwaka 2021 ambapo mahitaji ya gesi asilia katika mtambo huu yatakuwa takribani futi za ujazo milioni 46 kwa siku”. Amesema Dk. Kalemani.