Naibu Waziri wa Nishati Subira Mgalu ametoa wito kwa wananchi kuuza sehemu ya mazao waliyovuna ili waweze kulipia gharama za kuunganishiwa huduma ya umeme. Naibu huyo ametoa ushauri huo wilayani Bahi mkoani Dodoma alipokuwa akikagua utekelezaji wa mradi wa umeme ambapo ametaja gharama ya kuunganisha umeme huo wa REA kuwa ni Sh. 27,000. Mradi huo unatarajiwa kukamilika mwakani ambapo gharama za maunganisho ya umeme mpya zitakuwa Sh. 177,000 kwa umeme wa matumizi ya nyumbani.
Katika taarifa iliyosomwa na Meneja wa Shirika la Umeme (TANESCO) wilayani humo, Bryceson Kitila, imeelezwa kuwa kuna jumla ya vijiji 59 na kati ya hivyo 19 tayari vina huduma ya umeme huku vilivyosalia vikiwa katika mchakato wa kupata huduma hiyo.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Bahi Mwanahamisi Mkunda amesema maendeleo makubwa tayari yameanza kuonekana kutoka kwenye vijiji vyenye umeme ambapo wawekezaji wameanza kujitokeza na kuwekeza kwenye viwanda vya kukoboa mpunga katika baadhi ya vijiji.