Waziri wa Nishati, Dk. Medard Kalemani amesema ujenzi wa mradi wa umeme wa Rufiji ambao unatarajia kuzalisha megawati 2,115 utaanza rasmi tarehe 15 mwezi Juni mwaka huu. Waziri Kalemani amesema hayo baada ya kukagua miundombinu wezeshi ya mradi huo yaani umeme, maji, reli na barabara katika eneo utakapotekelezwa mradi huo wilayani Rufiji mkoani Pwani.
Katika ziara hiyo Dk. Kalemani aliyeambatana na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Constatine Kanyasu, Naibu Waziri wa Ujenzi, Elias Kwandikwa pamoja na makatibu wakuu kutoka wizara mbalimbali amesema mkandarasi amepewa miezi 36 ya ujenzi wa mradi huo na miezi sita ya maandalizi hivyo mradi unatarajiwa kukamilika Aprili mwaka 2022.
Akieleza kuhusu ujenzi wa miundombinu wezeshi ya mradi, Waziri huyo amesema kazi hiyo hadi sasa imekamilika kwa zaidi ya asilimia 80.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Constatine Kanyasu amesema wizara yake inaendelea na majukumu mbalimbali yatakayowezesha kuanza kwa mradi huo ikiwemo kusafisha sehemu itakayokuwa ni bwawa la kuhifadhia maji ya kuzalishia umeme.