Jumla ya Halmashauri 31 zimepatiwa vifaa vya kupima afya ya udongo kwa wakulima (Soil Scanner).
Vifaa vilivyogaiwa ni soil scanner, vishikwambi, printer, lamination machine pamoja na seti ya kompyuta katika Halmashauri za mikoa ya Kilimanjaro, Arusha, Manyara, Dodoma, Singida na Tabora.
Akizungumza wakati wa ugawaji wa vifaa hivyo, mwakilishi kutoka Ofisi ya Rais TAMISEMI, Dkt. Rehema Mdendemi ametoa wito kwa maafisa hao kutumia vifaa hivyo kwa ajili ya kutoa huduma kwa wakulima, hususan katika Halmashauri zao.
Dkt. Rehema ameeleza kuwa Serikali imeamua kutoa fedha kwa ajili ya kuimarisha huduma mbalimbali za ugani kama vile pikipiki na vifaa vya kupimia udongo kwa lengo la kuhakikisha kuwa mkulima anapata taarifa kamili za afya ya ardhi ya shamba lake kwa usimamizi mzuri wa Afisa Ugani.
“Serikali ina dhamira ya kuhakikisha kuwa Wakulima wanapata huduma bila changamoto zozote hivyo ni rai yangu kwenu kutunza vifaa hivi na kuvitumia kwa matumizi sahihi,” amesema Dkt. Rehema.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Msaidizi Sehemu ya Huduma za Ugani, Upendo Mndeme amesema kuwa zoezi hilo bado linaendelea katika Halmashauri za Mikoa mingine ambapo wataendelea kutoa elimu ya matumizi ya vifaa hivyo pamoja na zoezi la ugawaji kwa kila Halmashauri nchini.