Home VIWANDAUZALISHAJI Serikali yaweka mkazo kukuza tasnia ya ufugaji kuku

Serikali yaweka mkazo kukuza tasnia ya ufugaji kuku

0 comment 158 views

Mkutano wa Kwanza wa Tasnia ya Kuku na ndege wafugwao Kusini mwa Afrika umefanyika Tanzania ambapo Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko amehutubia mkutano huo.

Akimwakilisha Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Philip Isdory Mpango katika ufunguzi wa mkutano Oktoba 16, 2024 jijini Dar es Salaam, amesema kuwa ujio wa Mkutano unadhihirisha namna Tanzania ilivyokuwa na mahusiano mazuri ambayo yamefungua milango katika sekta mbalimbali ikiwemo ya tasnia ya kuku na ndege wafugwao.

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko.

Kupitia Jukwaa hilo, Dkt. Biteko ameiagiza Wizara ya Mifugo na Uvuvi kuanzisha mashamba ya kuku wazazi kwa ajili ya kuzalisha vifaranga, kuanzisha vituo vya kisasa, maabara pamoja na kuwekeza katika machinjio ya kisasa ya kuku.

Dkt. Biteko ametoa maagizo mengine ikiwemo “ Wizara iweke pia mfumo wa mnyororo baridi wa usambazaji wa kuku, iwekeze pia katika vizimba, chakula cha kuku na ianzishe viwanda vya kusindika vyakula vya kuku ili vipatikane ndani ya nchi na sio kutumia fedha za kigeni kuagiza nje,”

Ametaja faida za ufugaji kuku na ndege wafugwao kuwa ni pamoja na kuchangia usalama wa chakula na kuongeza pato la Taifa kikanda na kimataifa.

Amebainisha kuwa asilimia 55 ya kaya nchini na katika nchi mbalimbali ni ufugaji unaofanywa zaidi na wanawake na vijana na kuwa Tanzania ina kuku milioni 103.1 wakiwemo kuku wa asili na kisasa.

Ametoa wito kwa wadau wote wa ufugaji wa kuku kuendelea kushirikiana na Serikali kutekeleza majukumu yao kwa kuwa Serikali imetoa fursa kwa kila mmoja kuweza kujishughukisha na kujiongezea kipato.

Amekaribisha sekta binafsi kushiriki katika tasnia hiyo ili kusaidia kukuza uchumi wa nchi huku akiwataka watafiti kushirikiana na Serikali.

Akizungumza katika mkutano huo, Waziri wa Mifugo na Uvuvi Abdallah Ulega amesema kuwa kufanyika kwa mkutano huo ni matokeo ya mkutano wa Bodi ya Muungano wa Mapinduzi ya Kijani barani Afrika (AGRA) uliofanyika Dar es alaam na kuongozwa na Rais Dkt. Samia ambapo AGRA walielezwa juu ya kuipa kipaumbele sekta ya ufugaji wa kuku kwa kuwa nchini Tanzania familia nyingi zinafuga kuku.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Abdallah Ulega

“ Tunawashukuru AGRA na Food Alliance kwa kutukubalia na ndio maana leo jukwaa la kwanza limefanyika hapa Tanzania na kutoa fursa kwa wafugaji wetu kujifunza na kujenga mahusiano,” amesema Ulega.

Amebainisha kuwa takwimu zinaonesha kuwa ifikapo 2030 kuku watachangia asalimia 41 ya protini na kuwa watafiti nchini washirikiane na Serikali wanapotoa matokeo ili kutoleta taharuki kwa jamii kupitia matokeo ya tafiti zao.

“ Hivi karibuni watafiti walifanya utafiti kwa kutumia sampuli chache juu ya ulishaji wa kuku wanaofugwa na akina mama na vijana tafiti ile ilileta taharuki, kupitia Jukwaa hili nitumie fursa hii kuwaambia watafiti washirikiane na Wizara ili kutotoa taarifa za taharuki kwa jamii na kuwa Serikali inaweza kudhibiti wafugaji wasiofuata taratibu hivyo tusiharibu jitihada zinazofanywa na kukuza tasnia hii,” amesema Ulega.

“ Tunawaheshimu na kuthamini kazi zao ila tuone wanapofanya tafiti na kupeleka kwa jamii tuwe na mkakati wa pamoja wa kufikisha tafiti hizo kwa jamii,” amesisitiza Ulega.

Naye, Waziri Mkuu wa zamani wa Ethiopia na Mwenyekiti wa AGRA Dkt. Hailemariam Dessalegn, amesema kuwa fursa muhimu zilizopo kupitia ufugaji wa kuku ni chanzo cha protini, soko la uhakika na ajira kwa vijana na kushiriki katika mnyororo wa thamani.

Waziri Mkuu wa zamani wa Ethiopia na Mwenyekiti wa AGRA Dkt. Hailemariam Dessalegn.

“Jukwaa hili linatoa fursa ya kujifunza faida na changamoto katika tasnia hii na kuongeza ushirikiano. Kukuza tasnia hii katika nchi yetu inahitaji majukwaa kama haya na inahitaji utayari wa wadau mbalimbali kwa kuwa wana uwezo wa kuwekeza ili kukuza tasnia hii,” amesema Dessalegn.

Ameongeza “Tanzania ni kinara wa kuwa na njia shirikishi na ni imani yangu itaendelea hivi chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia ili kufikia ajenda ya Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs), haswa dhamira ya kumaliza njaa na umasikini ifikapo 2030. Hakuna nchi inayoweza kufikia mafanikio haya peke yake hivyo sera ya ukanda, mafunzo na majadiliano na mawasiliano ni muhimu kufikia malengo.”

Mfugaji kutoka nchini Malawi, Grace Gondwe amesema kuwa baada ya kumaliza Chuo Kikuu nchini humo alianzisha biashara ya ufugaji wa kuku wa kisasa licha ya kukutana na changamoto mbalimbali amemudu kufanya kazi hiyo kwa miaka mitano sasa na kuwa tafiti mbalimbali zinaonesha mahitaji yake yaongezeka siku hadi siku.

“ Kupitia ufugaji nimekuwa mshauri pia kupitia Kampuni yangu tumeanza kutumia teknolojia katika uzalishaji wa kuku ambapo uzalishaji umekuwa mkubwa kwa gharama nafuu. Vijana wenzangu napenda kuwaambia tuendelee kufuga kuku kuna fursa nyingi pamoja zinazoendana na ufugaji wa kuku,” amesema Grace.

Mfugaji wa kuku kutoka mkoani Tanga, Omary Mussa amesema ameanza ufugaji kupitia miradi mbalimbali na baada ya mafunzo amekuwa mfugaji tangu mwaka 2023 akianza na kuku 500 na sasa anafuga kuku 4,000 aina ya chotara na kuku wa kisasa.

“ Tanzania kufuga kuku ni utamaduni wetu tuna kazi ya kubadilisha kutoka kuwa tamaduni kuwa kibiashara nimeanzisha Kampuni ya Kuku Pesa Investment Group ili watu wafuge kuku kupata pesa,” amesema Mussa.

Ameongeza “ changamoto ni kuwa watu wanafuga bila faida, Kampuni yetu inatoa mafunzo kwa mtu anaye fuga ikiwa ni pamoja na kubadilisha mitazamo kuwa sio lazima uajiriwe unaweza kujiajiri mwenyewe. Hadi sasa vijana 108 wamepata mafunzo na ufugaji na tuna wafugaji 98 tunaowasimamia mkoani Tanga.”

Baadhi ya washiriki kutoka sehemu mbalimbali wakifuatilia Mkutano wa Kwanza wa Tasnia ya Kuku na ndege wafugwao Kusini mwa Afrika uliofanyika jijini Dar es Salaam.

 

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter